Hakuna mtu asiependa kuwa na uhusiano wa kimapenzi mzuri na wenye afya, mimi binafsi napenda sana kuona watu wanapendana, huwa napata maumivu na wakati mwingine hasira ninaposikia au kupata kesi ya uhusiano au ndoa kuvunjika.
Wakati wa kufundwa mara zote niliambiwa kuwa ukizubaa mapenzi kati yako na mumeo hayatokuwa kama mtakavyoanza hivyo basi unahitaji kuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna kuzoeana bali kujuana.
Sasa kwa vile Mfundaji mwenyewe alikuwa ni Hayati Bibi yangu aliezaliwa na kukua enzi za Mfumo Dume aliwakilisha somo kwangu kwa kusema “hakikisha unakuwa mstari wa mbele” lakini kutokana na maisha yalivyo sasa mimi nitasema kwako HAKIKISHENI (wake kwa waume) kuwa hamzoeani na badala yake mnajuana kiundani zaidi.
Uhusiano huwa mtamu kweli kweli unapoanza, hakuna hata mmoja kati yenu anaekumbushwa na mwenzie kufanya mambo/jambo, unajikuta tu unafanya mambo mazuri-mazuri kwa mpenzi wako, uhusiano unaendelea mnafikia mahali mnakubaliana kuishi pamoja part time(mf: mwisho wa wiki tu) au full time kwavile inakuwa ngumu sana kupitisha siku nzima bila kumuona Asali wa Moyo na baadae ndoa.
Baada ya kuishi pamoja au kufunga ndoa mmoja wenu au wote mnaanza kupunguza speed na hatimae inafikia mahali wote kwa pamoja mnajikuta mnadharau kufanya mambo mliokuwa mkifanyiana awali kwa sababu ya mapenzi......hatua hii ni mbaya sana na ndio huwa chanzo cha ugomvi au kutafuta mtu atakaekufanyia mambo bila kumkumbusha, hatua hii inaitwa KUZOEANA.
Baada ya kuzoeana na ku-miss hamasa, chachu ya mapenzi kutoka kwa mwenza wako, unaanza kulinganisha uhusiano wako na uhusiano wa watu wengine na kuanza kuona wivu na hata ku-wish kuwa mkeo au mumeo angekuwa kama yule au tungekuwa kama wale.