1.0
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge likijadili hoja ya
kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili jambo muhimu la dharura kwa mujibu wa
Kanuni ya 47 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2013, iliyowasilishwa na
Mhe. Said Nkumba, Mbunge wa Sikonge kuhusu Mgogoro kati ya Wafugaji na
Wakulima, Hifadhi na Uwekezaji, Mheshimiwa Spika alitoa Uamuzi ‘Speakers
Ruling’ kuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira ishughulikie kazi ya kutathmini na kuangalia jinsi Mpango wa
Kupambana na Majangili ulivyopangwa na
kutekelezwa na Serikali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Taarifa Rasmi za Bunge
za tarehe 1 Novemba 2013, wakati Bunge likihitimisha Hoja ya Kuairisha Shughuli
za Bunge, Mhe. Spika alitoa uamuzi ufuatao:-
…Kamati
ile ya kawaida ya Maliasili itaendelea na kazi yake ya kufanya tathmini ya
kuangalia jinsi mpango ule wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na ndani yake
itashughulikia kama kulikuwa na uzembe ama kuna watu wanahusika katika kuondoa
maisha ya watu kwa sababu za uzembe …
1.1
Kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Uchunguzi
Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi ulioutoa tarehe 01
Novemba, 2013 Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilikutana Dodoma tarehe
9 Novemba, 2013 kwa lengo la kujadili utaratibu wa kutekeleza jukumu hilo.
Katika kikao hicho Kamati iliazimia kuunda Kamati
Ndogo kwa mujibu wa Kanuni ya 117(18), ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Tole la
2013 ili iweze kushughulikia suala hilo kikamilifu.
1.2
Hadidu za Rejea, Wajumbe wa Kamati na muda wa kazi
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira kwa agizo lako la tarehe 01 Novemba, 2013, ilipewa Hadidu za Rejea
Nne (4) zifuatazo:-
1) Kutathmini na kuangalia jinsi Mipango ya
Kupambana na Majangili ilivyopangwa;
2) Kuangalia kasoro zilizojitokeza katika kutekeleza
mpango huo;
3) Kutathmini iwapo kulikuwa na uzembe katika
kutekeleza Operesheni Tokomeza ambao
ulisababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha na mali zao; na
4) Kuchunguza migogoro ya Ardhi inayohusu Wakulima,
Wafugaji na Wawekezaji kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi.
Mheshimiwa
Spika, Kamati hii ya uchunguzi iliundwa na Wajumbe Tisa (9) kama ifuatavyo:-
i. Mhe. James Daudi Lembeli, Mb.
ii. Mhe. Abdulkarim Esmail Shah, Mb.
iii. Mhe. Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
iv. Mhe. Kaika Sanin’go Telele, Mb.
v. Mhe. Dk. Henry Daffa Shekifu, Mb.
vi. Mhe. Amina Andrew Clement, Mb.
vii. Mhe. Haji Khatibu Kai, Mb.
viii. Mhe. Muhammad Amour Chomboh, Mb.
ix. Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa
Mheshimiwa
Spika, Sekretarieti iliyohudumia Kamati Ndogo ya Uchunguzi iliundwa na Wajumbe
wafuatao:-
i. Ndg. Theonest K. Ruhilabake
ii. Ndg. Gerald S. Magili
iii. Ndg. Chacha T. Nyakega
iv. Ndg. Stanslaus W.Kagisa
Mheshimiwa
Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
ilitakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti katika Mkutano wa Kumi
na Nne (14) wa Bunge. Hivyo basi, baada
ya uteuzi huo, Wajumbe wa Kamati Ndogo walipanga kuanza kazi tarehe 25 Novemba,
2013 na kuikamilisha ifikapo tarehe 15 Desemba, 2013.
1.3
Njia zilizotumika katika kukamilisha kazi
Mheshimiwa
Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
ilitekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Hadidu za Rejea ilizopewa kwa
kufanya rejea na kuzingatia yafuatayo:-
a) Kusoma na kuchambua nyaraka zilizoandaliwa na
Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuandaa na kutekeleza Operesheni Tokomeza
nchini. Nyaraka hizo ni hizi zifuatazo:-
i. Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept
Paper)
ii. Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
iii. Sheria ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge
(Na.3) 1988
iv. Sheria ya Wanyamapori (Na. 5) 2009
v. Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013
b) Kufanya mahojiano na watu mbalimbali:-
i. Waziri wa Maliasili na Utalii
ii. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
iii. Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
iv. Mkurugenzi Msaidizi Kikosi wa Dhidi ya Ujangili
v. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
vi. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za
Taifa (TANAPA)
vii. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA)
viii. Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Hifadhi za
Misitu (TFS)
ix. Mahojiano na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
c) Kuzuru maeneo yaliyoanishwa katika Taarifa ya
Wizara kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na yale yenye migogoro
kati ya Wakulima au Wafugaji na Wawekezaji katika maeneo ya hifadhi kwa lengo
la kuhakiki (verify) masuala yaliyoainishwa kupitia uchambuzi uliofanywa na
Kamati.
2.0
KUPOKEA NA KUCHAMBUA NYARAKA MBALIMBALI ZILIZOHUSU OPERESHENI TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, Hadidu Rejea ya kwanza iliitaka
Kamati Ndogo ya Ardhi, Malisili na Mazingira, kufanya tathmini na kuangalia
jinsi mipango ya kupambana na majangili ilivyopangwa. Ili kukamilisha jukumu
hilo, Kamati ilifanya yafuatayo:-
a) Kupitia na kuchambaua Mpango Kazi wa Operesheni
Tokomeza (Concept Paper) ulioandaliwa na Wizara
b) Kupitia na kuchambua Tathmini ya Utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza.
2.1
Uchambuzi kuhusu Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, katika kuchambua Mpango Kazi wa
Operesheni Tokomeza kwa lengo la kupata uelewa zaidi wa namna operesheni hiyo
ilivyopangwa na kutekelezwa, Kamati ilibaini kuwa, mpango huo uliandaliwa na
Wizara ya Maliasili na Utalii na ulikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Ukubwa wa tatizo la ujangili
ii. Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
iii. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
iv. Malengo ya Operesheni Tokomeza
v. Njia zilizotumika kutekeleza operesheni
vi. Maeneo ya operesheni na gharama za utekelezaji
vii. Tamko la Serikali kusitisha Operesheni Tokomeza
2.1.1
Ukubwa wa tatizo la ujangili
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, tatizo la
ujangili ni kubwa na limekuwa likisababisha idadi ya Tembo iendelee kupungua
nchini. Takwimu zinaonesha kuwa, idadi ya Tembo imepungua kutoka 350,000 (miaka
ya 1970) hadi kufikia 55,000 (mwaka 1989). Juhudi za kukabiliana na hali hiyo
kupitia Operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza idadi
ya Tembo hadi 141,000 (mwaka 2006) ingawa ilishuka tena hadi kufikia 110,000
(mwaka 2009).
2.1.2 Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali,
vitendo vya ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili
yafuatayo:-
i. Ujangili wa Kujikimu (subsistance poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha watu wenye kipato
kidogo na hulenga zaidi katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi
mahitaji mengine. Ujangili wa aina hii huathiri zaidi wanyama wanaoliwa na si
Tembo.
ii. Ujangili wa Biashara (commercial poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha zaidi watu wenye
uwezo mkubwa wa kifedha na hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa. Wanyama
wanaoathiriwa zaidi na aina hii ya ujangili ni pamoja na Tembo, Faru, Simba na
Chui.
Mheshimiwa
Spika, taarifa ilibainisha kuwa, kuongezeka kwa masoko
haramu katika nchi za Asia na Mashariki ya Kati ambayo yanatoa bei kubwa ya
nyara hizo, imekuwa ni chachu ya kuimarika kwa mitandao inayojihusisha na
ujangili (ndani na nje ya nchi) na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la vitendo
vya ujangili.
2.1.3 Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi waKupambana na
Ujangili ulilenga kujikita katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili wa
wanyamapori na misitu. Mpango huo ulioelezewa kuwa niwa muda mrefu na
kusimamiwa na kikosi kazi cha Taifa (national task force),umeanisha maeneo
yafuatayo kuwa ndiyo yaliyoathirika zaidi:-
i. Pori la Akiba Selous
ii. Hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba Maswa
na Pori Tengefu la Loliondo.
iii. Hifadhi ya Taifa Katavi na Mapori ya Akiba
Rukwa na Lukwati.
iv. Hifadhi ya Taifa Mikumi
v. Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za Taifa
Tarangire na Ziwa Manyara.
vi. Mapori ya Akiba Burigi, Biharamuro, Ibanda na
Rumanyika.
vii. Mapori ya Akiba Moyowosi, Kimisi, Ugalla na
Hifadhi ya Misitu Luganzo.
2.1.4
Malengo ya Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ambayo
ilizinduliwa rasmi tarehe 04 Oktoba, 2013 ilikuwa na malengo yafuatayo:-
i. Kuzuia vitendo vya ujangili ndani na nje ya
Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu, Mamlaka ya Hifadhi
Ngorongoro na Misitu ya Hifadhi na kufanya operesheni maeneo yote
yaliyoathiriwa na ujangili.
ii. Kuwatambua mapema majangili na kujua nyendo zao
ndani na nje ya maeneo ya hifadhi.
iii. Kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria wafanyabiashara haramu wa nyara za Serikali na mazao ya misitu.
iv. Kuvunja mitandao ya wafadhili, wanunuzi wadogo
na wakubwa pamoja na mawakala wa biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao
ya misitu.
v. Kufuatilia na kukamata mali za majangili
zilizotokana na biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu.
2.1.5
Njia zilizotumika kutekeleza Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, Mpango Kazi
wa Serikali kuhusiana na Operesheni Tokomeza, uliainisha kuwa operesheni hiyo
itaendeshwa kwa kutekeleza mambo yafuatayo:-
i. Kufanya uchambuzi wa kina wa watuhumiwa wa
mtandao wa ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa
mazao ya misitu.
ii. Kuwakamata watuhumiwa wote waliobainishwa kwenye
taarifa za kiintelijensia.
iii. Kupiga picha na kuchora ramani ya eneo la tukio
kwa kila mtuhumiwa (sketch map).
iv. Kuhoji na kuandika maelezo ya watuhumiwa wa
ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya
misitu.
v. Kukusanya na kuhifadhi vielelezo vyote
vitakavyokamatwa kutoka kwa majangili kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vi. Kuandika maelezo ya mashahidi na askari
wakamataji kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vii. Kuandaa mashitaka dhidi ya watuhumiwa na
kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
2.1.6
Maeneo ya Operesheni na gharama za utekelezaji
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza
ulianisha kuwepo awamu mbili za utekelezaji ambazoni; Mpango Kazi wa Muda Mfupi
na Mpango Kazi wa Muda Mrefu.
Katika Mpango Kazi wa Muda mfupi itafanyika
operesheni maalum katika maeneo yote ya ndani na nje ya hifadhi za wanyamapori
na misitu nchi nzima. Maeneo hayo yaligawanywa katika kanda 12 za utekelezaji
kama ifuatavyo:-
i. Selous, Mikumi, Udzungwa, Lukwika/ Lumesule na
Liparamba,
ii. Burigi/Biharamuro, Ibanda/Rumanyika na Rubondo,
iii. Moyowosi, Ugalla na Lugazo,
iv. Serengeti, Loliondo, Maswa, Ikorongo na Kijeshi,
v. Kilimanjaro, Arusha, Mkomazi/Umba, Simanjiro na
Longido,
vi. Tarangile, Manyara, Karatu/Ngorongoro,
Swagaswaga na Mkungunero,
vii. Rungwa, Ruaha, Mpanda – Kipengele,
viii. Rukwa, Lukwati, Katavi, Lwafi, Piti na Wembere,
ix. Mahale na Gombe,
x. Saadani na kwenye maeneo yenye misitu ya mikoko,
xi. Pori Tengefu la Handeni, Kilindi na Mkinga na
xii. Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe, Rufiji na
Mkuranga
Mheshimiwa Spika, ilianishwa kuwa, awamu ya kwanza
ya Mpango Kazi wa muda mfupi ingegharimu jumla ya Tshs. 3,968,168,667/= ambazo
zingechangwa na Taasisi za wanyamapori (WD, TANAPA, NCAA na TFS) kwa kila moja
jumla ya Tshs. 992,042,167/=
2.1.7 Tamko la Serikali kusitisha Operesheni
Mheshimiwa Spika, kufuatia michango na malalamiko ya
Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia hoja iliyotolewa na Mhe. Said Nkumba
Mbunge wa Sikonge, pamoja na maagizo ya Bunge kutaka Serikaliitoe maelezo
kuhusu hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali ilitoa Tamko la
kusitisha Operesheni Tokomeza tarehe 01 Novemba, 2013.
2.2
Uchambuzi wa Taarifa ya awali ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya awali kuhusiana na
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ilikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Washiriki wa operesheni
ii. Awamu za operesheni
iii. Mafanikio ya operesheni
iv. Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
v. Changamoto za operesheni
2.2.1
Washiriki wa Operesheni
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilihusisha
jumla ya washiriki 2,371 kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa mgawanyo
ufuatao:-
i. Wanajeshi (885) kutoka Jeshi la Wananchi wa
Tanzania,
ii. Askari (480) kutoka Jeshi la Polisi,
iii. Askari (440) kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili
(KDU)
iv. Askari Wanyamapori (383) kutoka Shirika la
Hifadhi za Taifa (TANAPA)
v. Askari (99) kutoka Wakala wa Huduma za Misitu
(TFS)
vi. Askari Wanyamapori (51) kutoka Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
vii. Waendesha Mashitaka (23) na
viii. Mahakimu (100
2.2.2
Awamu za Operesheni
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilipangwa
kutekelezwa katika awamu Nne (4) kama ifuatavyo:-
i. Awamu ya kwanza ambayo ililenga kusaka Silaha za
Kivita na Meno ya Tembo kutoka miongoni mwa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili.
ii. Awamu ya pili ambayo ililenga kusaka silaha
zisizomilikiwa kihalali na zile zinazomilikiwa kihalali lakini zinasadikiwa
kutumika kwenye vitendo vya ujangili.
iii. Awamu ya tatu, ambayo ililenga kutafuta yalipo
Maghala ya Nyara, kusaka Wafadhili na Wanunuzi wa nyara hizo na kuwabaini watu
wanaowakingia kifua wahusika wa vitendo vya ujangili.
iv. Awamu ya nne, ambayo ililenga kukamata Nyara
nyingine mbali na Meno ya Tembo na kuhakikisha watu walio katika makundi yafuatayo wanakamatwa:-
- Wawindaji haramu,
- Wavunaji haramu wa mazao ya misitu,
- Watu wanaolisha Mifugo ndani ya hifadhi, na
- Watu waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi
2.2.3
Mafanikio ya Operesheni Tokomeza
a) Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kutekelezwa
kwaOperesheni Tokomeza (tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi ilipositishwa (tarehe 01
Novemba, 2013) jumla ya kesi 687 zilifunguliwa zikiwahusisha watuhumiwa 1,030
katika maeneo yote kama ifuatavyo:-
i. Kanda ya Kwanza kesi 105 zikiwahusisha watuhumiwa
105
ii. Kanda ya Pili kesi 370 ambazo zilihusisha
watuhumiwa 375
iii. Kanda ya Tatu kesi 165 zilizohusisha watuhumiwa
498
iv. Kanda ya Nne kesi 47 zilizohusisha watuhumiwa 52
Mheshimiwa
Spika, hadi wakati Operesheni Tokomeza inasitishwa tarehe
01 Novemba, 2013 kati ya Kesi 687 zilizokuwa zimefunguliwa ni 132 tu ndiyo
zilikuwa zimetolewa maamuzi na 555 bado zilikuwa katika hatua ya
kusikilizwa. (Tazama Kiambatisho Na. 1)
i. Kukamatwa kwa meno ya Tembo 211 yenye uzito wa
kilo 522, meno ya Ngiri 11, Mikia ya wanyama mbalimbali 36, Ngozi za wanyama
mbalimbali 21, Pembe za Swala 46, Mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 Baiskeli
58, Pikipiki 8 na Magari 9.
ii. Kupungua kwa kasi ya mauaji ya Tembo kutoka
wastani wa Tembo wawili (2) kwa siku hadi tembo wawili tu katika kipindi chote
cha operesheni (siku 29).
iii. Hadi kufikia tarehe 11 Novemba, 2013 jumla ya
Bunduki za Kijeshi 18 zilikamatwa, Bunduki za kiraia 1579, Risasi 1964, Mbao
vipande 27,913, Mkaa Magunia 1242, Magogo 858 na Misumeno 60. Vyote hivyo vilikamatwa
katika Kanda ya Nne.
2.2.4
Changamoto za Operesheni Tokomeza
a) Vifo vilivyotokea wakati wa Operesheni
Mheshimiwa Spika,Taarifa ya Serikaliiliainisha vifo
kamachangamoto kubwa iliyojitokeza wakati wautekelezaji wa Operesheni Tokomeza
kutokana na watumishi 6 na watuhumiwa 13 kupoteza maisha. (Tazama Kiambatisho
Na. 2)
b) Hujuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikali ilifafanua
kuwa,utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulikumbwa na vitendo vya hujuma kutoka
kwa baadhi ya makundi ya jamii kama ifuatavyo:-
i. Mamluki miongoni wa washiriki wa Operesheni.
Mfano; kukamatwa kwa Askari Polisi na Askari Wanyamapori wakisindikiza gari
lenye Meno ya Tembo, na gari la Serikalikutumika kusafirisha Meno ya Tembo.
ii. Vyombo vya Habari kutumika kuvuruga operesheni
kwakueneza propaganda zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni hiyo.
iii. Baadhi ya wamiliki wa silaha kutuhumiwa kutoa
silaha zao ili zitumike kwa ajili ya vitendo vya ujangili.
C)
Tuhuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikai ilifafanua
kuwa,ingawa lengo la operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili
dhidi ya raslimali za Taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na tuhuma kadhaa
zikiwemo zifuatazo:-
i. Mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha
maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na hata wengine kupoteza maisha (Mfano;
Marehemu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo – Babati).
ii. Matumizi mabaya ya Silaha (Mfano; Mzee wa miaka
70 kuuawa kwa kupigwa risasi 3).
iii. Nyumba za wananchi kuchomwa moto (Mfano; Kijiji
cha Kabage Wilaya ya Mpanda – Katavi).
iv. Mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na
kupigwa risasi (Mfano; Ng’ombe 60 kuuawa kwakupigwa risasi).
v. Kukosekana kwa mwongozo wa utoaji wa taarifa
jambo lililosababisha viongozi husika wa Serikali kutopewa taarifa muhimu za
utekelezaji wa Operesheni. (Mfano; Waziri wa Maliasili naUtalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Waziri wa Ulinzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya).
vi. Askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu kukataa
kutoa ushirikiano wa kutosha pale walipohitajika kufanya hivyo.
vii. Kutoshirikishwa kwa viongozi wa Mamlaka za
Utawala katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
3.0
MAHOJIANO BAINA YA KAMATI NA WIZARA PAMOJA NA WABUNGE
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mahojiano na
makundi yafuatayo:-
i. Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi
zake
ii. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
iii. Waheshimiwa Wabunge
3.1
Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi
zake
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati
wanapata uelewa wa kutosha kuhusiana na Operesheni Tokomeza, Kamati liagiza
uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ukiongozwa na Waziri, kufika mbele ya
Kamati ili kueleza namna Operesheni Tokomeza ilivyoandaliwa na kutekelezwa hadi
ilipositishwa kupitia tamko la Serikali lililotolewa Bungeni tarehe 01 Novemba,
2013.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana na Waziri wa
Maliasili na Utalii pamoja na timu yake kwa siku tatu, tarehe 28- 29 Novemba,
na tarehe 01 Desemba, 2013. Katika vikao hivyo, Waziri aliieleza Kamati juu ya
Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza, raslimali (watu na fedha) pamoja na
tathmini iliyofanyika kwa kipindi ambacho Operesheni Tokomeza ilitekelezwa.
Mheshimiwa Spika, katika mahojiano na Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb na watendaji wake Kamati
ilifahamishwa yafuatayo:-
i. Kwamba Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi
kama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) akisema:
“…Operesheni ilikuwa ya kijeshi. Ilikuwa ya kijeshi kwa sababu ilitekelezwa kwa
amri ya jeshi Namba 0001/13 iliyotolewa tarehe 28 Septemba, 2013 na kusainiwa
na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi…”
ii. Kwamba, kinadharia inaonekana kwamba, Waziri wa
Maliasili na Utalii ndiye alikuwa Msemaji Mkuu, lakini kiuhalisia hakuwa
msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza kama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za
Bunge akisema; “…kinadharia inaweza ikasemekana kwamba mimi ndiye msemaji mkuu,
lakini mimi sikuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza …”
iii. Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisimamiwa
na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
iv. Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa
zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa
Maliasili na Utalii.
v. Operesheni Tokomeza iliingiliwa na Wanasiasa.
vi. Pamoja na Mpango kazi huo kuandaliwa na Wizara
ya Maliasili na Utalii, kwa namna ambayo haieleweki Waziri hakuuona wala
kuidhinisha rasimu ya mwisho ya Mpango huo. Hiyo ilidhihirika mbele ya Kamati
kutokana na Waziri kukiri kwamba hakuuona wala kuudhinisha
3.1.1
Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na
watendaji wa Wizara
Mheshimiwa Spika,kwa kutumia tathmini ya awali ya
nyaraka zilizowasilishwa pamoja na mahojiano na Waziri ilionekana kwamba,
Operesheni Tokomeza iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
kushirikiana na taasisi zilizo chini yake na kushirikisha vyombo vya Ulinzi na
Usalama.
Mheshimiwa Spika, licha Mpango wa Operesheni
Tokomeza kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, hata hivyo utekelezaji
wake ulisimamiwa na kuongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Hatua ya jeshi kuchukua jukumu la kuongoza
Operesheni Tokomeza, lilifanya viongozi wa Wizara kujiengua katika jukumu la
kuongoza (ead agency) na badala yake kuacha jukumu hilo kwa Jeshi pekee jambo
lililotafsiriwa kwamba, Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi.
Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano ilibainika
kwamba, hakukuwa na utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusiana na mwenendo
mzima wa Operesheni Tokomeza jambo lililofanya baadhi ya wahusika kutotambua
kikamilifu wajibu waokatika Operesheni hiyo.Mfano mzuri ni kwamba, licha ya kuelezwa
kwenye Kanuni za Utendaji (Operational Guidelines) za Operesheni Tokomeza
kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye atakuwa Msemaji Mkuu wa Operesheni
Tokomeza, bado Mhe. Waziri hakutekeleza jukumu hilo kwani alikwishatoa
mapendekezo katika rasimu kwamba Msemaji Mkuu awe ni Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aidha, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya Watendaji wa
juu wa Wizara walidaiwa kukwamisha utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa
Maliasili na Utalii kutokana na kuingilia mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi
ya Watumishi. Mfano ni majibizano kwa njia ya barua pepe kati ya Waziri na
Katibu Mkuu, Waziri na Mkurugenzi wa Wanyamapori na pia Katibu Mkuu na
Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa mujibu wa majibizano hayo Waziri anaonekana
kushangazwa na hatua ya Katibu Mkuu kuhoji hatua ya yeye kumuita mmoja wa
mtumishi wa Wizara ofisini kwake. (Kiambatisho Na. 3)
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa mfumo mzuri wa
kupashana habari kwa pande husika kuhusu mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza,
kulionekana kuathiri utaratibu mzima wa viongozi husika akiwemo Waziri wa
Maliasili na Utalii, kupata taarifa zinazotakiwa kwa wakati. Hali hiyo
ilichangia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kukumbwa na athari ambazo
zingeweza kuepukika iwapo kungekuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano pia Kamati
ilibaini uwepo wa hujuma kutoka kwa viongozi wa kisiasa na Serikali ambao kwa
namna moja au nyingine walionekana kuhusishwa na Operesheni Tokomeza ama wao
binafsi au ndugu zao.
Mheshimiwa
Spika, miongoni mwa hujuma ambazo Kamati ilizibaini
kupitia mahojiano naWaziri wa Maliasili na Utalii na Watendaji wake ni pamoja
na:-
i. Baadhi ya watuhumiwa wenye mahusiano na viongozi
wa kisiasa kutumia majina ya viongozi hao kuingilia utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza.
ii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kutuhumiwa
kujihusisha navitendo vya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali.
iii. Baadhi ya Mawaziri kutoa kauli zenye kuingilia
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. (Mfano: kutoa maelekezo kwa wahusika wa
Operesheni Tokomeza kwamba wasiguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote).
iv. Baadhi ya viongozi wavyombo vya Ulinzi na
Usalama kushiriki kudhoofisha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa
kusindikiza au kusaidia watuhumiwa wa ujangili kutoroka. (Mfano; viongozi wa
Polisi wa Wilaya na Mikoa)
Mheshimiwa Spika, kubainika kwa hujuma hizo ni
ishara tosha kwamba hata ndani ya Serikali yenyewe hakukuwa na dhamira ya dhati
kwa baadhi ya kwa viongozi na watendaji katika kuhakikisha vita dhidi ya
vitendo vya kijangili inapiganwa kikamilifu.
Hali hiyo ilisababisha utekelezaji wa operesheni
kukumbwa na athari nyingi kama vile; wananchi kupoteza maisha, mifugo kuuawa
kwa kuchomwa moto, njaa, kiu au kupigwa risasi), upotevu wa mali, nyumba
kuchomwa moto na vitendo vya ukatili dhidi ya wananchi ambavyo vilikiuka haki
za kibinadamu. Hali hiyo imesababisha utekelezaji wazoezi la Operesheni Tokomeza
kutafsiriwa kwamba ulilenga wananchi wasio na hatia na kuacha wahusika wa
ujangili.
3.2
Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 30 Novemba, 2013
Kamati ilikutana na kufanya mahojiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili
kubaini namna ilivyoshiriki katika Operesheni Tokomeza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dk. Emmanuel
Nchimbi, Mb alieleza kuwa, operesheni hii ilikuwa na lengo la kutimiza azma
(Commitment) ya Serikali iliyoitoa Bungeni kwamba, inakusudia kufanya
Operesheni ya kupambana na majangili.
Wizara yake ilishiriki kwa kutoa Askari Polisi 504
pamoja na baadhi ya vyombo vya usafiri na kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama
vya nchi vilikuwa vikikutana mara kwa mara kwa lengo la kuandaa mkakati wa
namna ya kushirikiana katika kutekeleza mpango huo wa vita dhidi ya ujangili.
Mheshimiwa
Spika,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alikiri kuwa, licha
ya lengo la operesheni kuwa zuri, kulijitokeza changamoto kadhaa zilizotokana
na baadhi ya washiriki wa operesheni kwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa
kama vile; ukatili dhidi ya mifugo na vitendo vya unyanyasaji wa wananchi kwa
kuwatesa kiasi cha kuwasababishia ulemavu wa kudumu au vifo.
Pia Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba, kutokuwepo
mfumo mzuri wa mawasiliano na Operesheni kuongozwa na jeshi, iliashiria kwamba
taarifa za operesheni zilikuwa zinakwenda kwa Mkuu wa Majeshi – CDF moja kwa
moja na hivyo kufanya pande zingine zinazohusika zisijue kinachoendelea.
3.2.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi na watendaji wake
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwepo
kwamawasiliano hafifu kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara nyingine
zilizoshiriki katika operesheni hii.Pia,kukosekana kwa mfumo mzuri wa mawasiliano,
kuliikosesha Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo iliandaa na kugharamia
Operesheni Tokomeza,fursa ambazo zingeiwezesha kufanya tathmini kuhusu
utekelezaji wa Operesheni hii.
Aidha, Kamati ilibaini kwamba, hatua ya
kutoshirikisha Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ililenga kutovujisha siri
dhidi ya watuhumiwa wa ujangili. Hatua hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa
viongozi wa mamlaka za utawala za Wilaya na Mikoa kutokana na kulaumiwa na
wananchi kwa kushindwa kuwasaidia pale walipokumbwa na matatizo.
3.3 Mahojiano baina ya Kamati na Waheshimiwa
Wabunge
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liliibukia
Bungeni baadaya wawakilishi wa wananchi
kupaza sauti kuhusu athari zilizowakumba wapiga kura wao, Kamati iliona ni
busara kuhoji baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii. Wabunge hao
walitoa taarifa muhimu kuhusu vitendo vilivyofanyika katika maeneo yao wakati
wa operesheni.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walieleza
kusikitishwa na namna ambavyo Operesheni Tokomeza ilikiuka malengo
yaliyokusudiwa na badala yake ikanyanyasa wafugaji kwa kuangamiza mifugo yao na
kuwaharibia mali zao kama vile; kuchoma moto nyumba, kupora fedha na vitu
vingine. Mbunge mmoja alinukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema:-
“…badala
ya Operesheni Tokomeza kusaka majangili, ikageuka kuwa Operesheni Tokomeza
Ufugaji…”
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliieleza
Kamati kuwa, siyo jambo la kawaida kwa watu wanaoagizwa kufanya jambo fulani
kwenda kinyume na maagizo.
Wakashauri kuwa, wahusika wote waliotenda kinyume
namaagizo wachukuliwe hatua stahiki ili kuepusha vitendo vya aina hiyo
visijirudie katika operesheni zitakazofuata. Pia Waheshimiwa Wabunge walishauri
kasoro zilizojitokeza zirekebishwe na operesheni iweze kuendelea ili kutowapa
mwanya majangili kujipanga upya.
3.3.1
Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, kimsingi Waheshimiwa Wabunge
wanaunga mkono Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kukomesha vitendo vya
kijangili na kunusuru raslimali za nchi hasa wanyamapori na misitu. Hata hivyo,
walieleza kusikitishwa na vitendo vilivyojitokeza wakati wa utekelezaji wa
operesheni na walisema haviwezi kuvumilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupata taarifa mbalimbali
kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, mahojiano na viongozi na watendaji wa Wizara na
kuzingatia taarifa zilizowasilishwa na Serikali, Kamati iliazimia kuzuru baadhi
ya maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza ili kufanya uhakiki.
4.0 KAMATI KUZURU MAENEO YALIYOATHIRIKA KWA
AJILI YA KUHAKIKI (VERIFICATION/OUTREACH)
Mheshimwa Spika, kutokana na wingi wa maeneo pamoja
na ufinyu wa muda, Kamati ilijigawa katika makundi matatu ili yaweze kutembelea
baadhi ya maeneo yaliyoainishwa katika Taarifa ya Serikali ili kufanya tathmini
(verification) kwa utaratibu ufuatao:-
4.1
Kundi la kwanza lilielekea Kanda ‘C’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Shinyanga, Kagera, Tabora, Kigoma, Rukwa, Katavi na Singida.
Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na Wajumbe
wafuatao:-
Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mb, Mheshimiwa Haji
Khatibu Kai, Mb na Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
4.2
Kundi la pili lilielekea Kanda ‘B’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Simiyu, Mara, Arusha na Manyara.
Mheshimiwa Spika,kundi hili liliundwa na wajumbe
wafuatao, Mheshimiwa Abdulkarim E. Shah,
Mb, Mheshimiwa Henry Daffa Shekifu, Mb na Mheshimiwa Amina Andrew Clement, Mb.
4.3
Kundi la tatu lilielekea Kanda ‘D’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Ruvuma na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na wajumbe
wafuatao; Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele, Mb, Mheshimiwa Muhammad Amour
Chomboh, Mb na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, ambaye hata hivyo hakushiriki
kutokana na dharura.
Mheshimiwa Spika,kama ilivyoainishwa hapo juu lengo
la Kamati kutawanyika Mikoani lilikuwa kutathmini athari zilizotokana na
Operesheni Tokomeza ambayo iliendeshwa nchini kuanzia tarehe 04 Oktoba, 2013
hadi tarehe 01 Novemba, 2013.
Mheshimiwa
Spika, ili kutimiza jukumu hilo kikamilifu, Kamati iliongozwa na taarifa
zifuatazo;
i. Mpango Kazi wa Operesheni Maalum ya kupambana na
Ujangili nchini,
ii. Taarifa ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
iliyotolewa na Serikali.
iii. Michango ya Waheshimiwa Wabunge kama
ilivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard).
iv. Madai yaliyotolewa na Wabunge kuhusiana na
athari zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
v. Maelezo yaliyotolewa na Mashahidi ambao
walihojiwa na Kamati.
vi. Vielelezo vilivyowasilishwa na Mashahidi
waliofika mbele ya Kamati.
5.0 MAKUNDI YA KAMATI YALIVYOTEKELEZA MAJUKUMU
YAKE
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili,
Kamati ilikutanana makundi yafuatayo:-
i. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
ii. Waheshimiwa Madiwani
iii. Waathirika wa Operesheni Tokomeza
5.1
Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikukutana na Kamati za
Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na kupokea taarifa iliyohusu hali ya
Ulinzi na Usalama hususan wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa Spika, kwa sehemu kubwa taarifa za Ulinzi
na Usalama za Wilaya zilisaidia kuanisha maeneo na matukio yaliyojiri wakati wa
Operesheni Tokomeza na athari zilizojitokeza. Wajumbe wa Kamati walitumia
uchambuzi wa taarifa hizo kupata uelewa zaidi kuhusiana na utekelezaji wa
Operesheni hiyo kabla ya kukutana na wananchi walioathirika ili kupata maelezo
zaidi.
5.2
Waheshimiwa Madiwani
Mheshimiwa Spika,katika baadhi ya Wilaya, Kamati
ilikutana nabaadhi ya Madiwani wakiwa ni wawakilishi wa wananchi katika ngazi
ya halmashauri ili kupata maelezo zaidi kuhusu utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza kabla ya kukutanana waathirika wa Operesheni.
5.3 Waathirika wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana nabaadhi ya
wananchi walioathirika na Operesheni Tokomeza na kupokea maelezo na malalamiko
yao kuhusu namna walivyoathiriwa na uekelezaji wa Operesheni.
Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya waathirika walitoa
ushahidi/vielelezo vya maandishi na picha ili kuthibitisha yale waliyokuwa
wakiyaeleza mbele ya Kamati. Wengine walikwenda mbali kiasi cha kuonesha
majerahana makovu waliyoyapata katika miili yao kutokana na mateso waliyopata
kwenye kambi maalum za mahojiano zilizoandaliwa na waendeshaji wa Operesheni
Tokomeza.
5.4 Kuzuru maeneo yaliyoathirika zaidi na
Operesheni
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata fursa ya kutembelea
baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na athari za operesheni Tokomeza kwa lengo la
kushuhudia mabaki ya vielelezo ili kujiridhisha iwapo tuhuma za athari
zilizotolewa kuhusu maeneo hayo zilikuwa zakweli.
6.0 YALIYOBAINIKA KATIKA ZIARA ZA KAMATI
6.1 Vikao na Kamati za Ulinzi na Usalama za
Mikoa/Wilaya
Mheshimiwa Spika, katika vikaona Kamati za Ulinzi na
Usalama za Mikoa/ WilayaKamati ilibaini kuwa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
haukushirikisha viongozi wa maeneo hayo ya utawala.
Kulikuwa na manung’uniko kwamba licha ya Wakuu wa
Wilaya na Mikoa kuwa wawakilishi wa Rais, waliachwa kando na Operesheni
kuendeshwa katika maeneo wanayosimamia hadi malalamiko ya wananchi waliokamatwa
yalipowafumbua macho kwamba walikuwa wanateswa na kufanyiwa vitendo vya
udhalilishaji na watekelezaji wa Operesheni. Aidha,
Kamati ilielezwa kwamba utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza ulisababisha hofu miongoni mwa wananchi na viongozi na kusababisha
baadhi yao kukimbia makazi. Mfano; Mkuu wa Wilaya ya Ulanga alikiri kujihifadhi
kwenye Hoteli moja nje ya Wilaya yake ambako alikutana na baadhi wananchi wake
waliokimbia adha za Operesheni Tokomeza.
Viongozi hao walieleza kwamba, kimsingi hawapingi
Operesheni Tokomeza Majangili kwaniililenga kunusuru raslimali za nchi hasa
wanyamaporina misitu visitoweke kutokana nakushamiri kwa vitendo vya ujangili.
Hata hivyo, walieleza kuwa hatua ya kutowashirikisha imelifanya zoezi hilo kuwa
na kasoro nyingi pamoja na udhalilishaji hata kwa viongozi waliochaguliwa na
wananchi.
6.2
Vikao vya Kamati na Waathirika wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mikutano
mbalimbali katika baadhi ya maeneo ilikofanyika Operesheni Tokomezakwa lengo la
kuwasilikiliza waathirika na kubaini mambo yafuatayo:-
Watuhumiwa kupekuliwa, kudhalilishwa na baadhi
kutojulikana walipo
i. Mheshimiwa Spika, badhi ya wananchi wakiwemo
viongozi, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na Watumishi wa Serikali
walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza. Baadhi ya
watuhumiwa waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru
maeneo hayo. Mfano; Vijana watatu wa Kijiji cha Osteti, Kata ya Chapakazi,
Wilayani Kiteto, walituhumiwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo. Vijana
hao ni Nyafuka Ng’onja, Ng’onja Kipana na Mswaya Karani.
ii. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai
kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake
kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao. Mfano; ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata
ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji
yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanae wa kiume (11)
akishuhudia.
Pia alidai kulazimishwa kuchora picha ya Chatu kwa
kutumia wembe kwenye paja lake. Vilevile, Bi. Neema Moses wa Babati alidai
kuvuliwa nguo na kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa
chupa sehemu zake za siri.
Aidha, baadhi ya akina mama walidai kubakwa na
kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja
alidai kubakwa na Askari wawili (2) wa Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya
usiku. Vilevile, mama mmoja mkazi wa Kata ya Matongo Wilayani Bariadi, alibakwa
na askari watatu (3) wa Operesheni Tokomeza Ujangili huku akiwa ameshikiwa
mtutu wa bunduki
iii. Watuhumiwa waliokamatwa walifanyiwa upekuzi
bila kuhusisha viongozi wa Serikali za maeneo husika na kutokuwepo kwa
mashahidi na hati za upekuzi.
Mfano; Ndg. Abdallah Pata na Bi. Flora Mwarabu wa
Kata ya Iputi Wilayani Ulanga na Ndg. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati,
walipekuliwa bila kufuata utaratibu.
Ukatili
na Udhalilishaji katika Kambi za Mahojiano
iv. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa
waliopelekwa katika kambi za mahojiano walidai kuteswa kwa adhabu zinazokiuka
haki za binadamu. Mfano; Diwani wa Kata ya Sakasaka wilaya ya Meatu Ndg. Peter
Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama
kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya
mapenzi na mti.
Mheshimiwa Spika, kutokana naukatili uliopitiliza,
baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile Guantanamo (Ruaha),
Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti).
Upotevu
wa mali za watuhumiwa na faini zisizoeleweka
v. Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, baadhi ya watuhumiwa walipoteza
mifugo, mali na fedha zao. Mfano; katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Iputi
mwananchi mmoja alidai kuporwa sanduku la VICOBA lenye shilingi laki saba na
nusu (750,000/=) pamoja na simu ya mkononi na Askari wa Operesheni Tokomeza
waliovamia nyumbani kwake. Vilevile Ndugu Musa Masanja wa Sakasaka Wilaya ya
Meatu, alidai kuporwa shilingi laki tatu 300,000/= pamoja na simu 2 za mkononi
na Askari Askari wa Operesheni.
Mheshimiwa Spika,Pia ilidaiwa kuwa mifugo ya
watuhumiwa ilikamatwa na kuingizwa ndani ya maeneo ya hifadhi na kufa kwa
kupigwa risasi au kukosa maji na malisho kutokana na kuzuiliwa kwa muda mrefu.
Baadhi ya mifugo ilitozwa faini bila stakabadhi au
stakabadhi kuonesha viwango vidogo ikilinganishwa na fedha halisi iliyolipwa.
Mfano:Ndugu Sosoma Shimula mwenye Ng’ombe 1700 Wilayani Kasulu alidai kwamba
alitakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni thelathini (30,000,000/=,
alipowasihi alipunguziwa hadi Milioni kumi na mbili (12,000,000/=) hata hivyo
aliweza kulipa Milioni kumi (10,000,000/=).
Alionesha Kamati stakabadhi inayoonesha kuwa amelipa
faini ya shilingi milioni moja tu (1,000,000/=). Stakabadhi hiyo ilijazwa
sehemu ya tarakimu, lakini hakuna kilichoandikwa katika sehemu ya kiasi cha
fedha kwa maneno. (Tazama Kiambatisho Na. 4)
Watuhumiwa
kuteswa na kuumizwa
vi. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa walidai
kupigwa na kuumizwa na askari wa Operesheni na wengine kupata ulemavu wa
kudumu. Mfano; katika Wilaya ya Itilima,Kijiji cha Mbogo Ndg Sita Rumala alidai
kupigwa na kuvunjwa mkono alionesha wajumbe mkono uliokuwa umefungwa bandeji ngumu
(P.O.P).
Aidha, Diwani Peter Samwel Ndekija wa Kata ya
Sakasaka, Wilaya ya Meatu, alidai kupigwa na kuumizwa vibaya mgongoni na
alionesha kwa wajumbe wa Kamati makovu aliyoyapata. Vilevile,ilielezwa kuwa
Ndugu Munanka Machumbe (24) ambaye ni bubu alipigwa risasi 3 zilizomjeruhi
mapajani na kuharibu sehemu za siri wakati akijaribu kuwahoji Askari wa
Operesheni kwa ishara sababu za kumtesa baba yake.
Aidha, katika tuko lingine Shekhe Mkuu wa Wilaya ya
Ulanga Ali Mohamed (70) aishiye kijiji cha Iputi, alidai kurushwa kichura na
kutandikwa bakora na Askari wa Operesheni Tokomeza. Pia,Ndg. Nyasongo Magoro Serengeti wa Kata ya Majimoto
wilaya ya Mulele alidhalilishwa mbele ya wananchi wake. (Tazama Kiambatisho Na. 5)
Mifugo
kuingizwa hifadhini na watuhumiwa kubambikwa kesi
vii. Mheshimiwa Spika,wakati wa Operesheni, mifugo
mingi ilikuwa hifadhinilakini hata ile iliyokuwa nje ya hifadhi iliingizwa na
askari wa hifadhi na wafugaji kutakiwa walipe faini ya shilingi Milioni tatu
(3,000,000/=) hadi Sita (6,000,000/=) kwa idadi ya ng’ombe 30 hadi ng’ombe 100
na aliyeshindwa kulipa faini mifugo yake iliuawa au kupigwa mnada na mfugaji
kufilisiwa.
Walioshindwa kulipa faini mifugo ilipigwa mnada na
wafugaji hawakuruhusiwa kununua wala kukaribia eneo la mnada, na katika mnada
mifugo iliuzwa kwa bei ya chini kuliko faini iliyotozwa Mfano; shilingi elfu
sitini (60,000/ =) kwa kila ng’ombe.
Watuhumiwa
kubambikwa kesi
viii.Ilidaiwa kwamba, baadhi ya watuhumiwa walidai
kubambikwa makosa ambayo hawahusiki nayo kama vile kumiliki silaha kinyume na
sheria, kukutwa na bangi au nyara za Serikalimfano; Bw. Elias Cosmas Kibuga wa
Gallapo Babati alidai kubambikiwa kesi ya kumiliki bunduki kukutwa na mkia wa
twiga kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, pia Bibi Zuhura Ali wa Kilombero
alidai kuteswa huku akilazimishwa kutoa silaha ambayo hakuwa nayo. Aidha, Bw.
Melkzedeck Abraham Sarakikya wa Itigi alidai kuteswa akilazimishwa atoe silaha.
Mateso
na vifo kwa Watuhumiwa
ix. Mheshimiwa Spika, baadhi ya wananchiwalidai kuwa
ndugu zao waliteswa kikatili kwa muda mrefu na bila kupatiwa huduma za lazima
kama chakula, maji na matibabu (siku 1 -2) hadi mauti yalipowafika. Kwa mfano
Ndg. Kipara Issa wa Wilaya ya Kaliua na ndugu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo,
Wilaya ya Babati.
Aidha, wananchi hao walidaikuwa mahojiano kwa
watuhumiwa yaliambatana na mateso makali kwa muda mrefu kiasi cha kusababisha
vifo. (Tazama Kiambatisho Na. 6).
Vilevile, watuhumiwa wengine waliodaiwa kupoteza
maisha wakati wa Operesheni Tokomeza ni Ndg. Wegesa Kirigiti wa Kijiji cha
Remagwe na Ndg. Peter Masea wa Kijiji cha Mrito (Tarime), Ndg. Mohamed Buto
(Masasi) na Gervas Nzoya (Kasulu).
Mheshimiwa Spika, pamoja na uthibitisho wa picha
zilizotolewa na wananchi kuhusu kuteswa hadi kufa kwa Bi Emiliana Gasper Maro,
Serikali kupitia Mkurugenzi wa Wanyamapori ilitoa Taarifa kwa Umma ikipinga
Taarifa iliyorushwa na kituo cha luninga cha ITV tarehe 19 Oktoba 2013 kuhusu
mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Askari wa kupambana na ujangili.
Taarifa hiyo ya Serikali inapinga kuwa Askari wa
Operesheni Tokomeza hawausiki na kifo cha mtajwa. Taarifa hiyo imeonekana
kukosa umakini kutokana na kujichanganya juu ya watu inaowazungumzia. Taarifa
hiyo inazungumzia majina mawili tofauti (Evelyn Gasper na Mariana Gaspar Mallo
wa eneo la Olongadiola) wakati muathirika halisi ni Bi. Emilliana Gasper Maro
wa Kijiji cha Orngadida, Gallapo.
(Tazama kiambatisho Na.7)
Ukatili
dhidi ya Wanyama
x. Mheshimiwa Spika, kuhusu vitendo vya ukatili kwa
wanyama ilidaiwa kwamba ng’ombe walipigwa risasi, na ndama walikufa kwa kukosa
maziwa kutokana na mama zao kukamatwa na kuzuiwa kwenye mazizi yaliyopo maeneo
ya hifadhi kwa muda mrefu. (Tazama Kiambatisho Na. 8)
Rushwa
kwenye Mapori ya Akiba
xi. Mheshimiwa Spika, Wananchi walidai kukithiri kwa
vitendo vya rushwa kwa watumishi wanaosimamia mapori ya akiba ya Maswa, Kigosi
Moyowosi, Burigi, Kimisi na Mkungunero kwa kutaja majina ya baadhi ya watumishi
wanaowatuhumu. Mfano; Ndg. Kileo mtumishiwa pori la Maswa, alidaiwa kuwa na
tabia ya kutoza wananchi faini bila stakabadhi au kutoa stakabadhi kinyume na
faini iliyotolewa au kutoa stakabadhi bandia.
Aidha, katika pori la Kigosi-moyowosi, watumishi
wafuatao walidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa; Ndg. Msocha, Alfred,
Kobelo na Odhiambo.
Aidha, ilidaiwa kuwa katika mapori ya Kigosi
Moyowosi na Kimisi zaidi ya wafugaji 100 wenye ng’ombe wanaokadiriwa kuwa
50,000 wanalipia kuchungia ng’ombe wao kwenye mapori hayo ya hifadhi tangu
mwaka 2000 kwa malipo maalum na hata Operesheni Tokomeza haikuwagusa.
Aidha, ilidaiwa kuwa Ndg. Msocha (Meneja wa Pori la
Akiba la Kigosi Muyowosi), alituhumiwa na baadhi ya wananchi kuwa amekuwa
akiwakodisha wafugaji hao kwa vipindi vya miezi mitatu, na wafugaji huruhusiwa
kulipa tena muda unapoisha. Aidha, Mfugaji ambaye hulipa kiasi kidogo
hulazimishwa kulipa huku akipigwa namifugo yake kuuawa kwa kupigwa risasi.
Ilielezwa kuwa, Wafugaji na Askari Wanyamapori
huwasiliana kwa simu ilil kutekeleza makubaliano ya malipo kwa malisho yao.
Nambaza simu zinazodaiwa kuwa za Askari Wanyamapori zimeorodheshwa. (Tazama
Kiambatisho Na. 9)
Mahusiano
kati ya wananchi na Askari wa mapori ya Akiba
xii. Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoishi kwenye
Mapori ya Akiba yanayo wazunguka walidai kuwa katika mahusiano mabaya na Askari
wa mapori hayo. Mfano;wananchi wa kijiji cha Kimotorok, Wilaya ya Simanjiro na
Askari wa pori la akiba la Mkungunero kiasi cha kufikia hatua ya kutishiana
maisha. Vitendo hivyo pia vipo kwa jamii zinazopakana na mapori ya Gurumeti.
Mahakama
na Magereza kuzidiwa uwezo
xiii.Mheshimiwa Spika, kutokana na Operesheni
Tokomeza ilidaiwa kuwa vyombo Mahakama na Magereza katika maeneo husika
vilizidiwa uwezo kutokana na wingi wa kesi na idadi ya Mahabusu. Mfano; Gereza
la Wilaya ya Bunda lenye uwezo wa kuchukua jumla ya wafungwa na mahabusu 217
lililazimika kuchukua hadi watu 411.
Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa wanalazimika
kusafiri umbali mrefu kuhudhuria kesi zao. Mfano; katika wilaya ya Serengeti
baadhi ya watuhumiwa walifunguliwa kesi Wilaya za Tarime, Bunda na Bariadi.
Watumishi
wa Umma kuhusishwa na Ujangili
xiv.Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa baadhi ya
Watumishi wa Serikali na vyombo vya dola (Polisi) wanajihusisha na ujangili.
Mfano ni Dereva wa OCD, Wilaya ya Ngorongoro aliyetuhumiwa kujihusisha na
ujangili wa Meno ya Tembo.
Askari huyo alihojiwa na viongozi wa Operesheni
Tokomeza katika kituo chake cha kazi. Vilevile, Ndg. Mohamed Ismail, Afisa
Wanyamapori (W) Meatu anatuhumiwa kukutwa na nyara za Serikali. Aidha,Askari
Polisi wawili (2 )Cpl. Isaack na PC Sixbert wa Mugumu Wilayani Serengeti
walikamatwa wakiwa na meno ya Tembo.
Mheshimiwa Spika, pia ilidaiwa kuwa baadhi ya
Maofisa wa Serikali wamekuwa wakitumia magari ya Umma ama kusafirisha au
kusindikiza watoroshaji wa nyara za Serikali. Mfano nigari la Serikali
lililokamatwa likifaulisha meno ya Tembo kutoka kwenye gari jingine huko
Mkuranga kwa lengo la kuyasafirisha kwenda Dar es Salaam.
Sambamba na hilo baadhi viongozi wa jeshi la Polisi
wametuhumiwa kusaidia watuhumiwa wa vitendo vya kijangili kutoroka na kuepuka
mkono wa sheria.
Migogoro
kuhusu mipaka ya Maeneo ya Hifadhi
xv. Mheshimiwa Spika, wananchi walidai kuwa baadhi
ya Mapori ya Akiba naHifadhi yamekuwa yakipanua mipaka yake bila kushirikisha
wananchi wa maeneo yanayowazunguka. Mfano; wananchi wa Wilaya ya Bunda
wanaopakana na Pori la Akiba la Gurumeti.
Pia, wananchi wa vijiji vya Kegonga na Masanga,
katika Kata ya Nyanungu, Wilayani Tarime wako katika mgogoro wa mpaka na TANAPA
wakidai kuwa bonde la Nyanungu limemezwa na eneo la Hifadhi kutokana na TANAPA
kuongeza mipaka yake bila kushirikisha wananchi wa maeneo hayo.
Aidha, katika Wilaya ya Ulanga kuna mgogoro katika
kata za Iputi na Lupiro dhidiHifadhi ya Selous.
Idara
za Wanyamapori katika Halmashauri kukosa vitendea kazi
xvi.Mheshimiwa Spika, kutokana na silaha za Idara ya
Wanyamapori katika baadhi ya Halmashauri kuchukuliwa wakati wa Operesheni
Tokomeza kwa ajili ya uchunguzi, wananchi wamedai kupata shida kutokana na
wanyama hasa Tembokuvamia mashamba na kuharibu mazao pamoja na kujeruhi au kuua
watu na mifugo.
Wanasiasa
kushawishi wananchi kuishi kwenye maeneo ya Hifadhi
xvii. Mheshimiwa Spika, wakati wa kutekeleza
Operesheni Tokomeza ilidaiwa kuwa nyumba na maboma ndani ya mapori ya akiba
zilichomwa moto. Mfano; Wilaya ya Sumbawanga kijiji cha Msila Kata ya Mfinga na
kijiji cha Kabage Wilaya ya Mpanda. Hata hivyo baadhi ya wananchi wameanza
kurejeakatika baadhi ya maeneo ya hifadhi kutokana na ushawishi wa wanasiasa.
Mfano; katika Pori la Hifadhi ya Jamii Ubende Wilaya
ya Mpanda walichangishwa shilingi laki moja (100,000/ =) kwakila kaya kwa ajili
ya kupatiwa huduma za kisheria iwapo mamlaka husika zitajaribu kuwaondoa ndani
ya hifadhi.
Aidha, Kamati ilipata taarifa kuwa, baadhi ya
viongozi wa Vyama vya Siasa wamekuwa wakigawa kadi za vyama vyao kwa wananchi
wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na kwa ahadi kwamba, vyama walivyojiunga nga
navyo vitawatetea wasiondoke katika maeneo hayo.
Tatizo
la Vibali vya Wakulima wa Muda
xviii. Mheshimiwa Spika, Kamati ilielezwa lipo
tatizo la raia wa nchi jirani kuingia nchini na kupewa vibali vyakuendesha
shughuli za kilimo(Peasant Permit)kwa muda, ambavyo hutolewa bilakubandika
picha ya mhusika/mwombaji hasa maeneo ya Karagwe.
Raia hao wanadaiwa kutumia nakala za vibali hivyo
kuingiza nchini wahamiaji haramu ambao baadhi yao huingiza makundi makubwa ya
mifugo hasa ng’ombe na wengine kutumia mwanya huo kuingiza silaha na
kujihusisha na vitendo vya ujangili katika baadhi ya mapori ya akiba. Mfano;
Pori la Akiba la Ibanda Rumanyika.
Vilevile kuna tatizo la majangili kutumia vivuli va
wafugaji kuingia kwenye hifadhi huku wakiwa wameficha silaha, na hivyo kuwepo
mazingira ya kushindwa kutofautisha kati ya majangili na wafugaji hususan
katika maeneo ya hifadhi ya Ruaha.
xix.Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro katika eneo la
Ushoroba (Buffer Zone) katika Kata za Lupiro, Mbugana Iputi Wilaya ya Ulanga,
maeneo ambayo jamii imejenga miundombinu kwa miaka mingi ikiwa ni pamoja na
shule, nyumba, mashamba, misikiti na makanisa huku Serikali ikiwa kimya kwa
muda mrefu.Hata hivyo, wakati wa Operesheni Tokomeza wananchi hao
walilazimishwa kuhama bila kuelekezwa waende wapi.
Michango
ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Operesheni
xx. Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya
michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia Hoja ya Mhe.
Saidi Nkumba haikuwa imefanyiwa utafiti wa kutosha kwani baadhi ya madai
waliyoyatoa hayakuwa na uhusiano na Oparesheni Tokomeza.
Kwa mfano;ni kweli kwamba ng’ombe 51 walitumbukia
katika mto Rubana Wilayani Bunda na kufa, hata hivyo tukio hilo lilitokea mwezi
April, 2013 ikiwa ni miezi 6 kabla ya Operesheni.
Aidha, ni kweli kuwa Wakazi wa Vijiji vya Kabage
Wilayani Mpanda na Luchima Wilayani Mulele walihamishwa kutoka katika maeneo ya
hifadhi na nyumba zao kuchomwa moto katika utaratibu uliofanywa na Halmashauri
hizo mwezi Septemba, 2013 kwa lengo la kuwapeleka kwenye maeneo rasmi ya
makazi.
7.0
MAONI NA USHAURI WA KAMATI KUHUSU TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI
TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati kuchambua nyaraka
husika kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, kuwahoji viongozi
mbalimbali wa Wizara na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kufanya ziara mikoani kwa
lengo la kuhakiki yaliyojiri kutokana na Operesheni Tokomeza, Kamati inapenda
kutoa maoni na ushauri ufuatao:-
i. Kwa kuwa, lengo la Operesheni Tokomeza lilikuwa
kunusuru raslimali za nchi hususani Wanyamapori na hasa Tembo na Misitu, na kwa
kuwa Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wameiunga mkono mbali na matatizo ya
kiutendaji yaliyojitokeza, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali
irekebishe haraka kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza ili kuendeleza na kukamilisha awamu zote za operesheni kama zilivyo
kwenye mpango na kunusuru raslimali za Taifa hasa wanyamapori na misitu ambayo
inatishiwa kutoweka kutokana na vitendo vya ujangili.
ii. Kwa kuwa,Kamati imejiridhisha kwamba matatizo na
upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza yamechangiwa na
maandalizi mabaya ya Mpango kazi ambao Waziri Mwenye dhamana hakuidhinisha, na
kwa kuwa, imedhihirika kuwepo hali ya sintofahamu (kwa mujibu wa hansard)
iliyosababishwa na watendaji wakuu wa Wizara kwa makusudi kuamua
kutomshirikisha kikamilifu Waziri katika hatua za mwisho za maandalizi ya
Mpango kazi, hivyo basi Bunge linaazimia kwamba, Serikali iwachukulie hatua
stahiki za kinidhamu Wasaidizi Wakuu wote wa Waziri walioshiriki katika Mpango
kazi huo.
iii. Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba pale Jeshi la
Wananchi (JWTZ) linaposhirikishwa katika Operesheni ufanisi mkubwa hupatikana,
na kwa kuwa, bado iko haja ya kuendeleza Operesheni Tokomeza kwa maslahi ya
Taifa, na kwa kuwa ushahidi wa mazingira ‘circumstantial evidence’ unaonesha
kuwa Jeshi lilichukua uongozi wa operesheni baada ya kugundua kuwa washiriki
kutoka Vikosi vingine (Polisi, TANAPA, TSF na NCAA) kwa kushirikiana na
wafugaji wenye ushawishi wa kifedha pamoja na wanasiasa, walihujumu operesheni
hiyo kwa kutoa taarifa kwenye mtandao mkubwa wa kijangili ambao umejengeka
kuanzia Wizarani hadi kwenye maeneo ya Hifadhi na kusaidia ‘majangili papa’
wasikamatwe, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:-
- Serikali kuchukua hatua za makusudi kuuvunja
mtandao huo na pia;
- Kuandaa operesheni nyingine ambayo itapangwa na
kutekelezwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa.
iv. Kwa kuwa, kumekuwepo na operesheni kadhaa kabla
ya Operesheni Tokomeza ambazo zililenga kupambana na ujangili, na kwa kuwa,
Operesheni Tokomeza imeshindwa kupata mafanikio yaliyotarajiwa, na kwa kuwa,
ushahidi wa mazingira unaonesha wazi kwamba, Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU)
kimeshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali
iimarishe kikosi hicho kwa kukifanyia tathmini na kukiunda upya ikiwa ni pamoja
na kukiwezesha kwa rasilimali (Watu, fedha, magari, silaha za kisasa na vifaa
vya mawasiliano kama redio na simu).
Serikali iunde chombo ambacho kitakuwa na jukumu la
kusimamia na kutathmini utendaji kazi wa KDU.
Iwapo utaratibu huo utazingatiwa ni wazi vitendo vya ujangili
vitadhibitiwa bila kutumia operesheni kubwa kama Uhai na Tokomeza.
v. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa vitendo vya
utesaji na ukatili wa hali ya juu, ukiukwaji wa haki za binadamu na uzembe
miongoni mwa Askari wa Operesheni Tokomeza (ushahidi wa wahusika upo), hali
ambayo imesababisha baadhi ya Wananchi kupoteza maisha, kupata ulemavu wa
kudumu pamoja na kupoteza mali zao. Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:-
- Serikali Iwabaini wote waliohusika na vitendo vya
kinyama, mateso na udhalilishaji dhidi ya watuhumiwa, iwachukulie hatua stahiki
na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hili katika Mkutano ujao wa
Bunge.
- Ifanye
tathmini ya kina kwa kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kujua athari za
Operesheni hii na kutafuta njia ya kutoa kifuta machozi kwa waathirika, ili
kurejesha imani ya Wananchi kwa Serikali yao.
vi. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Operesheni
Tokomeza ilikuwa haikutengewa fedha katika Bajeti ya Wizara ya Maliasili na
Utalii katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kwa kuwa kiasi cha fedha Tshs.
3,968,168,667/= kilichopatikana kutoka Idara na Mashirika Tanzu ya Wizara
haikutosheleza mahitaji ya fedha ya Operesheni Tokomeza kutokana na ukubwa wa
eneo la Operesheni, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali itenge Bajeti
Maalum ya kutosheleza mahitaji ya Operesheni Tokomeza.
Serikali kutenga Bajeti kwa ajili ya kuendeleza
shughuli za uhifadhi katika maeneo ya Hifadhi ikiwa ni pamoja na kuweka
raslimali watu ya kutosha na miundombinu mingine muhimu.
vii. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Taarifa kwa Umma
iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori tarehe
23 Oktoba 2013, haikuwa sahihi na pia ililenga kuudanganya Umma kwa kuficha
mazingira na sababu za kifo cha Bi Emilliana Gasper Maro, hivyo basi, Bunge
linaazimia kwamba, Serikali ichukue hatua za kumwajibisha Mkurugenzi wa Idara
ya Wanyapori kwa kuudanganya umma kwa kujaribu kuficha ukweli.
viii.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa kumekuwapo
mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya Maafisa Wanyamapori, Maafisa Misitu
katika mapori ya akiba, Misitu ya Serikali na katika baadhi ya Hifadhi za Taifa
wa kupokea rushwa, kutesa wananchi, kuwabambika kesi na kujihusisha na
ujangili,na kwa kuwa Kamati inayo majina na vielelezo vya wahusika, hivyo basi,
Bunge linaazimia kwamba, Serikali ifanye tathmini nchi nzima kwa lengo la
kutambua kiwango cha vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi hao, na
kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu wale watakaobainika kuhusika ikiwa ni
pamoja na kuwawajibisha na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
ix. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa baadhi ya
viongozi wa kisiasa na Serikali waliingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
kwa manufaa yao binafsi, kwa mfano, agizo la kuwataka wahusika wa Operesheni
Tokomeza kutowagusa Viongozi wa Kisiasa wa ngazi zote, kauli ambayo
ilitafsiriwa kuathiri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kubagua Watanzania
katika makundi ya Viongozi na Wananchi wa kawaida, hivyo basi, Bunge linaazimia
kwamba, Serikali ihakikishe kuna uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua
kutekeleza jambo la Kitaifa kama Operesheni Tokomeza.
x. Kwa kuwa, Kamati imethibitisha kuwa, baadhi ya
wanasiasa wamekuwa wanawadanganya wananchi waliothibitika kufanya shughuli za
uchumi kwenye maeneo ya hifadhi, na kuwaahidi kuwatetea pindi Serikali
inapochukua hatua za kuwaondoa katika sehemu hizo, ikiwa ni pamoja na kuwapa
kadi za vyama vyao vya siasa, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, serikali
ihakikishe kwamba, wananchi hawaendeshi shughuli za kiuchumi kwenye maeneo ya
hifadhi na kuwaonya wanasiasa waache kuwalaghai wananchi kwa maslahi yao binafsi.
xi. Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba katika baadhi
ya maeneo ya mipakani mfano Karagwe,
Idara ya Uhamiaji hutoa vibali kwa raia wa nchi
jirani vya kuishi na kulima hapa nchini, vibali ambavyo havina udhibiti
wala tija kwa nchi, na kusababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima
na wafugaji lakini pia uharibifu wa mazingira kwa kuingiza mifugo hifadhini,
hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali isitishe mara moja zoezi la kutoa
vibali hivyo, kufuta vilivyopo na kuwataka raia hao wa kigeni wenye vibali kuondoka Nchini mara moja.
xii.Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba zaidi ya
asilimia 25 ya eneo la Nchi ni hifadhi,
namipaka ya maeneo mengi yaliyohifadhiwa haijaainishwa, na kwa kuwa Serikali
haina uwezo wa (raslimali watu na fedha) wa kusimamia na kulinda mipaka ya
maeneo haya kikamilifu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali kufanya
yafuatayo:-
• Kuridhia Idara ya Wanyamapori na Wakala wa Huduma
ya Misitu kuajiri idadi ya watumishi wanaotakiwa kama Serikali bado inaendelea
kuyahifadhi maeno hayo.
• Kuainisha mipaka ya mapori yote ya akiba, hifadhi
za taifa na Misitu ya Serikali kwa alama maalumu na za kudumu ili kuepusha
Wananchi kuingia katika maeneo hayo kwa kutojua mipaka.
• Kuyaachia mapori ya Serikali ambayo yamekosa sifa,
ili yatumike kwa kilimo na ufugaji kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya
ardhi.
xiii.Kwa kuwa,yapo maeneo ya mapori na Hifadhi
ambayo yana migogoro ya muda mrefu ambapo wananchi wameishi katika maeneo hayo
kwa muda mrefu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali irekebishe mipaka
husika au iwahamishie Wananchi hao
kwenye maeneo mengine yenye miundombinu. Serikali iwaagize Mawaziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii na Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kutembelea maeneo yote yenye migogoro nchini na kuitafutia
ufumbuzi ili wananchi waweze kuelewa hatma yao katika maeneo hayo kwani
wamekuwa katika hali ya sintofahamu kwa muda mrefu.
xiv.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa migogoro
baina ya Wananchi, Wawekezaji na hifadhi katika maeneo ya Meatu, Tarime, Bunda
na ile ya Loliondo na Kimotorok ambayo inashughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu,
hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe inamaliza (kama
ilivyoahidi) migogoro iliyopo Loliondo na Kimotorok na maeneo mengine mapema
iwezekanavyo.
Kurekebisha haraka kasoro zote za kisheria
zilizokiukwa kwa makusudi na Idara ya Wanyamapori kiasi cha kusababisha mgogoro
baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu na mwekezaji katika Pori la Hifadhi ya
Jamii la Makao pamoja na kuwawajibisha Watendaji wa Idara ya Wanyamapori
waliosababisha mgogoro huo.
xv.Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba, migogoro
wanayokumbana nayo wafugaji kutokana na kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi
pamoja na kero nyingine ni kutokana na kukosekana kwa miundombinu sahihi na
endelevu kwa ajili ya ustawi wa mifugo, na kwa kuwa, Mheshimiwa Rais aliunda
Wizara mahsusi kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini akitambua umuhimu
wa Sekta hii kwa uchumi wa Taifa, na kwa kuwa, Tanzania ni ya pili kwa wingi wa
mifugo Barani Afrika, ni wazi kwamba adha wanazokumbana nazo wafugaji ni
matokeo ya kutokuwepo sera na mipango madhubuti ya muda mfupi na mrefu.
Hivyo basi, Bunge linaishauri Serikali kumtaka Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kujipima na kuona iwapo bado anastahili
kuendelea kuhodhi wadhifa alionao.
xvi.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa baadhi ya madai
yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge Bungeni wakati wakichangia Hoja ya Mhe.
Saidi Nkumba ilikuwa ni ya kweli; na kwa kuwa yaliyoelezwa katika madai hayo
hayana uhusiano na Operesheni Tokomeza kwani yalitokea kabla ya Operesheni
hiyo; hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Waheshimiwa Wabunge kuwa makini
zaidi na kufanya utafiti kwa lengo la kuhakikisha michango yao inakuwa sahihi
na inalenga hoja mahsusi iliyo mbele ya Bunge.
8.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, jukumu uliloikabidhi Kamati hii
lilikuwa zito na lilihitaji umakini mkubwa na muda wa kutosha katika
kulitekeleza. Kutokana na ufinyu wa muda na mazingira magumu wakati wa
kutekeleza jukumu hilo, Kamati inakiri kwamba haikuweza kutembelea maeneo yote
yaliyoathirika na zipo lawama kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba, Kamati
haikuweza kupita katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapenda kuwahakikishia
wananchi wote kuwa, kupitia taarifa mbalimbali za viongozi na wawakilisihi wa
waathirika mbele ya Kamati, malalamiko yao yamezingatiwa na kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika maelezo
yetu ya utangulizi, Kamati inaamini na kote tulikopita wananchi wanakiri kuwa,
lengo na azma ya Serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili lilikuwa jema
kwani lililenga kunusuru maliasili zetu kwa ajili ya maendeleo endelevu na
heshima ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini maelezo yote
yaliyotolewa na wananchi pamoja na viongozi wao yalikuwa na dhamira njema.
Aidha, mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yanalenga kuisaidia Serikali kuchukua
hatua za makusudi na haraka kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ili kuepuka kutokea kwa vitendo
vinavyoashiria ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na Utawala Bora nchini.
Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe binafsi
kwa dhati kutokana na kuiamini Kamati yangu na kuikabidhi jukumu hili zito. Hii
ni ishara tosha kwamba una imani na Wabunge wako na kwamba wanaweza kufanya
kazi kwa niaba yako.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe shukrani za dhati kwa
Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Didimu Kashilillah, kwa kuiwezesha Kamati hii
kufanya kazi yake vizuri na kuikamilisha kwa wakati. Aidha, kwa namna ya pekee
napenda kuwashukuru makatibu walioihudumia Kamati hii wakiongozwa na Ndugu
Theonest K. Ruhilabake ambao ni Ndugu Gerald Magili, Ndugu Chacha Nyakega na
Ndugu Stanslaus Kagisa.
Aidha, ninapenda kuwashukuru viongozi wa Mikoa,
Wilaya, Kata na Vijiji ambao walionyesha ushirikiano mkubwa Kamati
ilipotembelea maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu
Kamati inawashukuru watumishi wafuatao; Ndugu Silva Chindandi, Ndugu Ndigwako
Mwaigaga, Ndugu Victoria Mizengo, Ndugu Germina Magohe na watumishi wengine
ambao kwa namna moja au nyingine walishiriki katika kuihudumia Kamati hii hadi
inakamilisha taarifa hii.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
James
Daud Lembeli, Mb
MWENYEKITI
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA
0 comments: