Leo tutazungumzia kanuni za mafanikio kwa wajasiriamali.
Katika shughuli au biashara yoyote unayofanya au unayotarajia kufanya, ni
lazima uwe na mtazamo sahihi au mtazamo chanya ili ufanikiwe. Ujasiriamali una
kanuni zake ambazo ni muhimu sana kuzijua na kuzifuata ili kuyafikia mafanikio
ya kweli. Kama ukishindwa kufuata kanuni hizo basi uwezekano mkubwa ni kwamba
hutaweza kufanikiwa kupitia ujasiriamali.
KANUNI ZA UJASIRIAMALI
Kama tulivyowahi kueleza katika matoleo yaliyopita, ili ufanikiwe katika
ujasiriamali kama ilivyo katika shughuli nyingine yeyote, lazima ufuate kanuni
na misingi iliyowekwa. Kinyume na hapo, mafanikio huwa magumu sana. Zifuatazo
ni baadhi ya kanuni ambazo ukizifuatilia, utafanikiwa kupitia ujasiriamali.
1. Kuthubutu
Hii ni kanuni muhimu sana kwa mjasiriamali, hapa tunazungumzia uwezo na utayari
wa kufanya maamuzi magumu ya kuingia katika biashara fulani au mradi fulani
huku ukiwa umeondoa nidhamu ya woga. Watu wengi ni waoga wa kuchukua hatua au
kuthubutu kuingia katika biashara, mradi n.k.
Wengi wanaogopa hasara, kuanguka mtaji au kufilisika. Mjasiriamali bora ni
lazima awe na uwezo wa kuthubutu kufanya mambo makubwa lakini uthubutu huo
uendane na utafiti wa kina. Usiwekeze sehemu ambayo hujafanya utafiti wa
kutosha.
2. Nidhamu
Hii pia ni kanuni muhimu sana kwa mjasiriamali. Nidhamu ni muhimu sana katika
biashara, matumizi ya pesa, muda, nidhamu kwa wateja na kila kitu kinachohusu
shughuli zako zinazokuingizia kipato. Nidhamu ni chanzo cha mafanikio kwani
ndiyo inayosimamia sehemu kubwa ya biashara zako.
3. Umakini
Wale waliofanikiwa sio tu walikuwa tayari kufanya kazi bali waliweka umakini
mkubwa katika kazi walizokuwa wakifanya. Mjasiriamali anatakiwa kuwa makini kwa
kila jambo, anatakiwa kujua soko linaendaje na pia ni lazima awe na uelewa wa
kutambua mabadiliko yanayojitokeza katika soko, uzalishaji na uendeshaji kwa
jumla.
4. Uwezo wa kusimamia
Mjasiriamali lazima awe na uwezo wa kuongoza na kusimamia biashara yake na
kutoa uamuzi sahihi mara zote. Katika ujasiriamali, uwezo wa kusimamia na
kuwaongoza watu wa chini yako ni muhimu sana kwani hata kama ukianza na
biashara ndogo, lazima baadaye itakuwa kubwa hivyo utalazimika kuajiri watu
wengine wa kukusaidia.
Endapo utakosa uwezo wa kuwasimamia, ni dhahiri kwamba watakuibia, watafanya
kazi tofauti na ulivyotegemea na mwisho utaanguka kibiashara.
5. Kujituma bila kusukumwa
Ili ufanikiwe katika biashara yoyote, lazima uwe na moyo wa kujituma na uipende
kazi unayoifanya. Usisubiri kusukumwa kwa sababu hakuna atakayefanya kazi hiyo.
Jifunze kuwahi kuamka asubuhi ili uendane na kasi ya soko, jitume kufanya mambo
ambayo yataiboresha biashara yako bila kuchoka na fanya kazi kwa moyo wako
wote.
6. Uaminifu
Uaminifu ni silaha kubwa itakayokulinda mjasiriamali na kuwafanya watu wengi
wapende kufanya biashara na wewe. Jifunze kulipa madeni hata kama ni madogo
unapodaiwa, wauzie wateja wako huduma au bidhaa kwa bei halali, lipia kodi na
vibali vyote muhimu. Kamwe usiwauzie watu bidhaa zilizokwisha muda wake, zenye
ubora hafifu au mbovu kwani kwa kufanya hivyo, wateja watakukimbia na huo ndiyo
utakuwa mwisho wa biashara yako.
Hakika mtu anayefanikiwa lazima awe na sifa hizo zote hapo juu.
ReplyDeletekaribu kwa wanaohitaji mikopo isiyohitaji dhamana ya hati yoyote
na isiyokuwa na riba BONYEZA HAPA