Makala hii
inachambua mambo matano ambayo huwa ni mzigo mzito kwa wajasiriamali , na pia
makala inaonyesha baadhi ya njia za kukabiliana na changamoto hizo.
Ubia: Mara
nyingi imekuwa ni ngumu kwa watu wengi kufanya biashara kwa kushirikiana na
watu wengine, hususani katika hatua za mwanzo za uanzishwaji wa biashara.
Vikwazo vinavyojitokeza katika kufanya ubia na watu wengine ni vingi kama vile
:
Kutokupata
watu waaminifu, Kupata watu wasio na moyo wa kujitolea kufanya shughuli za
biashara yenu, kupata watu wanaokuwa wagumu kujitolea mtaji wa kutosha kufanya
biashara yenu, na zaidi sana, kupata watu wasio na muelekeo au mtazamo wa mbali
wa kijasiriamali, yaani wao wanawaza faida ya haraka haraka, na kwamba kwao
biashara ni sehemu ya kuingiza fedha ya ziada tuu ya leo au kesho.
Usimamizi wa
wafanyakazi: Mambo magumu yanayojitokeza katika usimamizi wa wafanyakazi ni
wafanyakazi kukosa uaminifu na kuwa na ufanisi wa chini ya kiwango.
Usipoangalia utapata hasara, na hata kupoteza wateja kwani wateja kwa ujumla
huja kufuata bidhaa na huduma zako ambazo zinatolewa na hao wafanyakazi.
Dawa yake:- Kuna namna
kadhaa za kupambana na tatizo hili. Hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe kujenga
muundo mzuri wa biashara yako ikiwa pamoja na mpango bora wa kifedha ili uweze
kulipa wafanyakazi kwa kiwango cha kuridhisha.
Ukishakuwa
na mpango mzuri wa kifedha maana yake utaweza pia kuajiri watu wanaokidhi
kiwango cha kazi unachotaka wafanye, na sio basi tuu ili mradi watu.
Muundo wa
biashara:
Hili limekuwa ni tatizo kwa watu wengi hususani wafanyabiashara wadogo na wa
kati. Ni tatizo zaidi kwakuwa wafanyabiashara wenyewe wengi hawaoni kama ni
tatizo, wakitoa visingizio kuwa eti uendeshaji wao wa biashara ndio muundo bora
zaidi.
Hapa
nazungumzia kuwa na biashara ambayo haina mgawanyiko wa majukumu, haina
mchanganuo wa biashara, haina utunzaji sahihi wa taarifa, na wala haifuati
taratibu za kisheria kama usajili, kuwasilisha taarifa za fedha , kulipa kodi,
kuwa na akaunti benki, n.k.
Dawa yake:-Kama
haufahamu jinsi ya kuunnda muundo imara wa biashara yako, mkodi mtu
akufanyie kazi hiyo, au jifunze ili uweze kufahamu namna ya kuweka muundo vema.
Heshimu taaluma za watu, na omba ushauri inapobidi.
Fanya bidii
uzungukwe na wafanyakazi unaowaamini na wenye uzoefu na ujuzi wa kile
wanachokifanya. Jifunze mambo mengi zaidi kuhusu usimamizi wa biashara, na kuwa
macho na changamoto unazokumbana nazo kwani hizo zinakupa mafundisho ya
kuboresha biashara yako.
Mtaji: Kikwazo
hiki hujitokeza katika mitazamo mitatu, kwanza wakati wa kutaka kuanzisha
biashara, pili wakati biashara imeshaanza ila fedha hazitoshi kuendesha vema,
na tatu pale mfanyabiashara anapokusudia kupanua biashara yake.
Dawa yake: Ili
kukabiliana na kikwazo cha mtaji yafuatayo yanaweza kusaidia,
Kuanza
biashara kidogo kidogo: Hii namaanisha kuwa kufikiria namna ambazo unaweza kuanzisha
biashara kwa mtaji mdogo na wakati huo huo ukafanya kwa ufanisi. Hii inaweza
kwa kuchunguza kwa umakini gharama zisizo za lazima, mambo ambayo unaweza fanya
wewe mwenyewe au kusaidia na watu wengine bila kuajiri, pia chunguza aina ya
bidhaa ambazo kweli ni za lazima kuanza nazo.
Kutunza
taarifa za biashara yako kwa ufasaha na kuwa na muundo bora wa uongozi, hii itakusaidia
kuwa kutimiza masharti ya benki, na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ambao
wanaweza kukuongezea mtaji.
Zingatia pia
kuwa na mali zisizohamishika, na pia kuna na mahusiano mazuri na wadau
mbalimbali kwani wao wanaweza kuwa vyanzo vya kukupatia mtaji. Mfano Badala ya
kununua bidhaa kwa fedha taslimu, unaweza kukopa- mtaani tunaita "Mali
Kauli".
Ushindani wa
kibiashara: Kikwazo hiki kinajitokeza kwa namna nyingi ikiwa ni pamoja na
uwezekano mkubwa wa kuigwa na watu wengine. Ni kawaida watu kutaka kuiga kama
ufanyavyo hasa pale unapoonekana kufanikiwa.
Dawa yake:- Jifunze
kusoma alama za nyakati, kwa kufuatilia habari zaidi zinazohusiana na aina ya biashara
unayofanya, wafahamu wapinzani wako vema, soma taarifa pia za mambo ya kijamii,
kimataifa, siasa na hata burudani, vyote hivi vinaweza kukupa muelekeo wa mambo
katika jamii hivyo kujituma zaidi na wewe kubadilika.
0 comments: