Kuna kitu kimoja ambacho
naamini masikio huwa yanasikia hata macho kuona, lakini moyo siku zote huwa
haukubali. Leo tuuandae moyo kukubaliana na jambo ambalo huamini kuwa
haliwezekani:
Ni
jambo gani?
Jambo hilo ni kuachwa.
Katika uhusiano wa kimapenzi ambao siyo rasmi, kuna matukio mengi ambayo
huwafanya baadhi ya watu kusikia kauli lakini moyo usikubali.
Ni kauli gani?
Kuna walioniuliza kuwa inapotokea mmoja katika uhusiano anamweleza mwenzake: “Mimi na wewe mapenzi basi.” Je, atajuaje kama mtamkaji anamaanisha?
Ukitaka kujua kama anamaanisha utaona mawasiliano hasa ya simu yanakuwa ya shida tofauti na zamani. Hataonyesha ushirikiano na hata ukitaka kujua sababu majibu yake yanakuwa ya kiburi.
Wengi wanateseka sana kufikia hatua ya kuchanganyikiwa kutokana na wapenzi wao kutowaeleza sababu za msingi za kuvunjika kwa penzi lao.
Kwa kawaida mtu akikuambia ‘sikutaki’ na akiwa anamaanisha, unatakiwa kuachana naye, lakini kwa udhaifu wa wanadamu tuna tabia ya kubembeleza ili kuhakikisha tunayamaliza na kurudi katika hali ya kawaida.
Kwa vile penzi lenu halikuwa na macho, anayelivunja kuna kitu alijiandaa zamani ndiyo maana hakuonei huruma.
Nini cha kufanya?
Kama amekueleza ‘hakutaki’ lakini bado ukafanya bidii ya kumbembeleza na ikashindikana, ilihali macho yameona, masikio yamesikia, inabidi kukubaliana na kilichotokea hata kama ulimpenda. Kumbuka hakuwa abiria katika safari ya maisha yako.
Moyo utakubali?
Unatakiwa ujifahamu wewe ni nani na kutambua kuwa kumpata mpenzi wako haikuwa kama kuokota kitu. Kama nilivyowahi kusema kuwa mapenzi ni bahati, elewa uliyemchagua au aliyekuchagua hakuwa bahati yako.
Ukishafahamu hilo, fanya kama mfanyabiashara aliyetegemea faida lakini amepata hasara ambayo hawezi kuing’ang’ania, bali atabadili mwelekeo.
Penzi linalokutesa ni biashara ya hasara ambayo ni lazima uibadilishe. Nina uhakika utampata uliyemkusudia, hakuna aliyeumbwa duniani kuumia milele.
Faraja nyingine zinatafutwa, usikate tamaa, jipange upya, ueleze moyo wako kwamba, aliyepita hakuwa sahihi kwako.
0 comments: