Makala
hii inalenga kuibua tafakari ya namna bora ya kutafuta ajira na kuanzisha
shughuli binafsi za kijasiriamali. Ingawa ni kweli kuwa kuhitimu ngazi fulani
fulani za elimu ni jambo la msingi katika kupata ajira au kuwa na shughuli
imara za kijasiriamali, wengi wamejikuta ngazi zao za elimu haziwasaidii
kukabiliana na changamoto za ajira na ujasiriamali.
1. Boresha uwezo wako wa ufasaha wa
lugha : Lugha ndio msingi mkuu wa mawasiliano. Jikite vema
katika Kiswahili fasaha, na kiingereza kinachofuata kanuni sahihi katika
kuongea na kuandika. Haijalishi una kiwango gani cha elimu, fanya bidii
kuboresha uwezo wako wa kuandika vema na kuongea. Tumia hata internet kutafuta
namna bora za kuboresha uwezo wako wa kuongea na kuandika kwani ‘broken’
english haitokufikisha popote, na Kiswahili kisichofuata kanuni hakitokufanya
watu wakuchulie ‘serious’ katika maamuzi yao ya kufanya kazi nawe, iwe
kibiashara au kiajira.
2. Jikite katika ujuzi fulani:
Kama unataka kuitegemea elimu yako kuzalisha huduma au bidhaa fulani, ni lazima
basi uwe kweli na ujuzi wa uhakika katika jambo fulani, na sio tuu kuwa na cheti. Tafakari kwa umakini
katika vyeti ulivyo navyo, ni mambo gani haswa unaweza kuyafanya kwa ufasaha,
jikite katika hayo, ili kuwa na ujuzi imara utakaokupa heshima na kukubalika
mbele ya wateja wako watarajiwa. Zaidi sana kumbuka, unaweza kujifunza ujuzi
mpya usiokuwepo katika vyeti vyako.
3. Jitangaze :
Kupitia mtandao wako, kupitia mikutano mbalimbali unayohudhuria iwe ya
kifamilia, kidini, marafiki au vikundi vingine, hakikisha watu wanatambua uwepo
wako , na kuwa wanajua kuwa unao ujuzi fulani. Zaidi sana sio tuu wajue unao
ujuzi fulani, bali wajue pia kazi ulizokwisha fanya kupitia ujuzi fulani ulio
nao. Watambue pia kuwa upo unapatikana kama utahitajika kwa ajira au
kibiashara. Mitandao kama Facebook, inaweza pia kutumika kujieleza uwezo wako.
4. Jenga mtandao wa watu
mbalimbali: Kuwa karibu na watu mbalimbali ili
uweze kujifunza mengi toka kwao, na pia watu hao wanaweza kuwa wa msaada mkubwa
kwako kama wateja wako, au wasambaji wa bidhaa fulani unazohitaji. Pia watu
katika mtandao wako wanaweza kukusaidia kupata mtaji wa kuanzia ujasiriamali
wako. Hata hivyo kumbuka, watu wamsingi katika kujenga nao mtandao wanahitaji
kukutambua wewe kama mtu muhimu kwao pia, hivyo jiweke kama mtu muhimu kwa
kuonyesha uadilifu, ujuzi wako, na heshima kwa wengine. Soma zaidi jinsi ya
kujenga mtandao imara bofya hapa
5. Kuwa mbunifu:
Tambua kuwa kinachowafanya watu kununua bidhaa fulani ni kwakuwa wanaamini
bidhaa hiyo itakidhi hitaji lao. Hivyo basi tumia muda wako kuangalia matatizo
au changamoto katika jamii na jinsi unavyoweza kuleta suluhu za changamoto
hizo. Sio lazima uzalishe bidhaa mpya kabisa, hata kusaidia kuleta huduma adimu
sehemu fulani, kusaidia kuboresha utendaji kazi wa watu kwa huduma za kiakili
unazoweza kutoa kama ushauri, ni moja ya ubunifu unaoweza kufanya. Kumbuka
ubunifu si jambo la haraka, unahitaji muda kusoma mazingira, fani na watu,
kisha utafakari namna unavyoweza kutumia ufahamu wako wa mazingira, ujuzi
mbalimnbali, na tabia za watu, ili kuleta huduma au bidhaa itakayohitajika na watu.
6. Fikra sahihi: Kila mmoja wetu ana njia ya kipekee ya
kufikia mafanikio yake maishani. Ingawaje ni kweli kuwa ajira na biashara
zinatuingizia kipato cha kujikwamua kimaisha, hakuna kanuni moja ya namna gani
utaingia katika ajira au biashara ili ufanikiwe kama fulani. Hivyo basi ,
usijilinganishe na watu wengine, kubali kuwa maisha yako ni ya kipekee, fikiria
hali uliyo nayo kuwa ni ya kipekee na inahitaji suluhu ya kipekee. Hivyo tafuta
njia yako ya kipekee ya kujiajiri kwa kuangalia hobbies zako, mtandao
wako, ujuzi wako n.k. Pengine hata
kutokupata kwako kazi ni kwa sababu unawaza kupata ajira kama fulani na fulani
walivyopata, au unawaza aina fulani ya kazi ndiyo ‘itakayokutoa’ kimaisha.
Kumbuka kuna baadhi ya watu wana degree mbili na hawana kazi nzuri zaidi ya
watu wenye degree moja, na kuna watu waliishia darasa la saba tuu, ila wana
kipato kizuri na maisha bora.
7. Ota kwa usahihi na ujiamini:
Hata kama unahisi hali yako kimaisha sio nzuri, bado unahitaji kuweka picha
kubwa ya maisha yaliyo bora hapo baadae. Kuota sahihi ni kufikiria kwa umakini
nini hasa unapenda kufanya, nini hasa unatamani yawe mafanikio yako, na zaidi
sana kuota huku kunakuwezesha kujiona kabisa umefikia hali husika unayoitamani
kwani unaamini na kujiamini kuwa zipo njia za kufikia huko. Kuota na kujiamini
ni muhimu kwani ndiko sikuzote kutakako kusukuma kuendelea na unachofanya hata
kama unapitia magumu, ndio wahenga walisema “palipo na nia, pana njia”. Ukiota vema na ukajiamini, hautokaa tuu bure
bure, ukilalamika ajira ngumu, au hauna mtaji, badala yake utatafuta mbinu za
ziada, na kuwa mbunifu kwakuwa unakitu kinachokusuma kukifikia katika maisha
yako, na hasa ndoto hiyo ikiwa inajumuisha kuleta mabadiliko katika maisha sio
tuu, mabadiliko kwa maisha yako peke yako, bali kwa jamii pia.
0 comments: