Baadhi ya watu wamekumbwa na tabia
ya kuahirisha mambo ya msingi bila kuwa hata na sababu ya msingi ya kuahirisha
huko. Wengine ni uvivu wa kuanza au kuendeleza jambo fulani. Zipo sababu nyingi
kwa nini uvivu au kuahirisha huko hutokea. Wengine huwa ni kisingizio maarufu
cha kuwa wapo ‘bize’ sana, wakati wengine ni kwa sababu ya kujiachia- yaani
kuridhika na hali waliyo nayo sasa).
Makala hii inachambua mambo matano
(5) ambayo ukizingatia unaweza kushinda uvivu, kuridhika na kuahirisha hairisha
mambo ya msingi bila sababu ya msingi:-
1. Weka
picha ya maisha mapya: Fikiria vile maisha yako yatakavyobadilika kutokana
na kufanikiwa katika jambo ambalo sasa unakuwa mvivu kulifanya au unalifanya
kwa kusua sua. Pengine maisha yako
yatabadilika kwa kuongeza mtandao wa watu muhimu katika maisha yako, pengine
kipato chako kitaongezeka, pengine jina lako litakua na sifa kwako zitaongezeka,
pengine utajitengeneza uhuru wa fikra n.k
2. Tambua
wajibu ulionao kwa watu wako wa karibu: Jambo la msingi unaloona uvivu
kulifanya au kuliendeleza kiasi kwamba unajikuta unaahirisha mara kwa mara,
linaweza kuwa watu walio karibu nawe wanakutarajia ulifanye. Mfano , pengine
umetoa ahadi ya kufanya jambo husika, pengine ni jukumu la kikazi, pengine
jukumu la kibiashara, kifamilia, au hata
jukumu la kimapenzi (kuwa kufanya kwako jambo husika kutatimiza matarajio ya
mpenzi wako).
3.Tambua
wajibu wako wa kiroho: Kumbuka pia una jukumu la kiroho la kutenda mambo ya
msingi na kuwa mtu wa msaada kwa wanaokuzunguka na dunia kwa ujumla. Haijalishi
wewe ni wa dini gani, sote tuna jukumu la kuwa wa msaada kwa wenzetu. Hivyo
kama kuanza au kuendeleza jambo unalotakiwa kufanya – iwe kujiendeleza kwako
kielimu, kuanzisha biashara,kubadili tabia fulani iwe bora zaidi, n.k , tambua kufanya hivyo hakutakunufaisha
wewe peke yako, bali kutanufaisha wengi.
4.Fikiria
‘maadui’ zako: Kumbuka kuwa kuna watu ambao
wangependa kukuona haufanikiwi, hawa ni ‘adui’ zako. Hivyo kwa kadri
unavyoahirisha mambo yako ya msingi au kuwa mvivu katika kuanza na kukamilisha
mambo hayo, tambua unatengeneza nafasi za ‘ushindi’ kwa adui zako.
5.Jiambie
unaweza: Ukiwa na
mashaka ya kuweza kuanza au kuendeleza jambo unalolitamani au kulitafakari
itakuwa ngumu pia kuanza jambo husika. Hivyo kujikuta ukiahirisha au kuwa mvivu
tuu wa kuanza na kuanza au kuendeleza jambo husika. Watu wengine wanaweza
‘kukupa moyo’ katika jambo fulani, hata hivyo wewe mwenyewe ni muhimu ujione
–utengeneze picha ya akilini , kuwa umekamilisha jambo husika kwa mafanikio.
0 comments: