Elimu ni
mchakato usioisha wa upataji maarifa. Mtu anaweza kupata maarifa kwa njia rasmi
au isiyo rasmi. Elimu rasmi ni ile tunayoipata kutoka kwenye taasisi za elimu
kama vile mashule. Elimu isiyo rasmi ni aina ya elimu ambayo haimlazimu mtu
kwenda shule. Inaweza kupatikana muda wowote na popote.
Lengo kubwa la
elimu ni kutengeneza maisha bora kwa watu. Tunapozungumzia elimu ya
ujasiriamali tunamaanisha elimu inayotilia mkazo katika kufikiri kwa ubunifu
katika kutumia fursa zilizopo kwa lengo la kutengeneza ajira ambazo husaidia
katika ustawi wa kijamii na ukuaji wa uchumi. Hii ndiyo aina ya elimu ambayo
inaweza kuyafanya maendeleo ya taifa kuwa endelevu. Maendeleo endelevu ni aina
ya maendeleo yanayokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Ni aina ya maendeleo ambayo hayatikisiki upesi
bali yanaweza kudumu na kuhimili vikwazo vya, kijamii kisiasa na kiuchumi.
Nchini Tanzania elimu ya ujasiriamali inahitajika sana ili kuzitumia kwa
ufanisi fursa na raslimali zilizopo. Tanzania imejaliwa maziwa, mito, bahari,
mabwawa n.k. ambayo siyo kwamba yamejaa samaki tu bali yamejaa pia viumbe
wengine kama vile viboko, mamba n.k.
Nchi imejaliwa
ardhi kubwa ambayo haijatumika, misitu na wanyama mwitu na wale wa kufugwa. Pia
nchi imejaliwa kuwa na gesi na madini kama vile almasi, dhahabu, Tanzanite,
makaa ya mawe kwa uchache tu. Hata hivyo, vitu vyote hivi havijatumiwa
kikamilifu ili kuleta maendeleo ya watu. Kwa maneno mengine, tunakosa maarifa
na ujuzi wa kiujasiriamali katika kuzibadilisha fursa hizo kuwa maendeleo.
Iwapo tunataka maendeleo endelevu lazima tutengeneze/ tuandae watu ambao
wanaweza:
• Kuendeleza
bidhaa mpya
• Kugundua
huduma na njia mpya zinazotilia mkazo matumizi halisi katika kiwanda au shirika
• Kugundua na
kutumia masoko mapya ambayo kiwanda au shirika halijayatumia
• Kugundua na
kutumia nyenzo mpya za utoaji raslimali ambazo hazijawahi kutumika
• Kuwa tayari
kupambana na hatari yoyote kwa faida ya nchi
Nini
kifanyike?
Ili kuwa na
elimu ya ujasiriamali yenye ufanisi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya mtu
mmoja mmoja na nchi kwa ujumla, mambo yafuatayo inabidi yafanyike:
•
Mihtasari/programu na moduli za elimu ya ujasiriamali ni lazima ziwe na malengo
ya kuendeleza ari ya ujasiriamali kwa wanafunzi (kujenga motisha na ufahamu).
Hii inajumuisha kuendeleza uwezo wa kijasiriamali ili kuweza kubainisha na
kutumia fursa zilizopo, kuwapatia wanafunzi ujuzi unaohitajika katika kuanzisha
biashara na kuziendesha ili zikue. Katika hali hizi zote, ni muhimu
kuwahamasisha wanafunzi ili waweze kufikiri na kutenda kama wajasiriamali na
pia ili wawe wenye kuwajibika kimaadili na kijamii.
• Ujasiriamali
ni sharti ufundishwe na wataalamu ambao wanafahamu jinsi ya kulifundisha somo
hili. Inapaswa
kufahamika kwamba ujarisiarimali ni vitendo na kwamba ili kuwapatia motisha
wanafunzi, njia/mbinu mbalimbali za kufundishia inabidi zitumike. Kwa mfano, ni
muhimu somo la ujasiriamali lifundishwe na wajasiriamali wenye moyo wa kufanya
hivyo. Mbinu ya kuiga ni muhimu zaidi katika ufundishaji wa ujasiriamali kwa
sababu watu hupenda kumsikiliza yule wanayemwamini na yule aliyefanya kitu
kwenye jamii.
• Shule ni
sharti zifungamanishwe na kazi. Uhusiano huu wa shule na kazi husaidia
kupunguza
matarajio ya
kazi kwa vijana na pia husaidia kupunguza tatizo la ajira kwa wasomi
walioajiriwa na wale wasio na ajira.
Elimu ya
ujasiriamali umeleta mabadiliko makubwa tangu kuanza kwake. Ijapokuwa mtu
anaweza kuwa na sifa za ujasiriamali, ni sharti afundishwe somo hilo ili
kumpatia maarifa na ujuzi wa kushindana katika ulimwengu kwa ujumla wake.
Ufundishaji makini wa ujasiriamali utawezesha kupatikana kwa maendeleo endelevu
na hivyo kuwawezesha watu kuwa na maisha mazuri katika nchi zao.
0 comments: