Kila mtu ana mawazo ya kufanikisha kitu fulani.
Mawazo hayo baadae huzalisha malengo, na kwa kujiwekea malengo ndio njia ya
kufanikiwa katika yale tunayotaka kufanikisha. Kuwa na haja ya kutimiza lako
jambo ndio chachu itakayokupelekea wewe kuyaendea yako malengo bila kusita.
Kwakuwa hakuna kitu tunachoweza kufanikisha bila kukifanyia kazi basi ni wazi
kuwa hatuna budi kuwajibika ili kutimiza malengo yetu.
Leo napenda
kuongelea malengo ya muda mfupi yani malengo ya kukamilisha kwa siku hii ya
leo. Siku ya leo ina saa 24 kama zilivyo siku nyingine ila unaweza kufanya siku
ya leo kuwa ni bora na yenye tija kuliko zote katika maisha yako.
Maisha ni namna tunavyoishi kila siku, moja wapo ya
kitu kinachotuletea maendeleo ni kazi na shughuli mbalimbali za kimaendeleo
tunazofanya kila kukicha mpaka jioni. Unaweza kufanya mengi sana uliyoazimia
kukamilisha kwa siku ya leo, jinsi utakavyotumia muda wako vizuri kwa kufanya
yale unayotaka kutimiza kwa siku ya leo ndivyo utakavyopata mabadiliko makubwa
na yenye tija katika kazi zako za siku.
Tumia
hizi mbinu mbinu (2) kufanikisha mengi kwa siku ya leo.
1.
Panga kazi zako katika hatua ndogo ndogo.
Ili kuepusha mrundikano wa kazi nyingi ambazo
nyingine ni kubwa kwako kuweza kufanya kirahisi, ni vyema ukazivunja kazi zako
katika hatua ndogo ndogo. Panga kufanya kila kazi katika muda wake. Jiwekee
malengo ya kutekeleza kazi zako kidogo kidogo na kuzifanya kwa ufanisi na
uhakika.
Ikiwa utaamua
kupanga utekelezaji wa kazi zako kwa mpangilio mzuri itakusaidia kurahisisha
kumaliza kazi hizo ndani ya muda maalum uliojiwekea. Jua ni kazi gani utafanya
kwa dakika 20 na ipi utaimaliza baada ya saa 2 nakadhalika. Kama kila kazi
utaifanya kwa wakati wake ipasavyo utaweza kuepuka usumbufu wa mrundikano wa
viporo vya kazi ambao sio wa lazima.
2.
Weka kipaumbele mambo yako ya msingi unayotaka kukamilisha kwa siku ya leo.
Ni muhimu sana kupanga siku yako mapema kabisa na
kwa kuzingatia uhalisia wa kazi au shughuli zenyewe. Pima uzito wa kazi zote unazotegemea kufanya kwa siku ya leo iwe
nyepesi au nzito andika chini kwenye karatasi na jipange namna ya kutekeleza
kazi zako, panga kwa makini kazi zako kwa kujua zipi zitachukua muda mfupi
kukamilisha na zipi zitachukua muda mrefu.
Katika
kuandika malengo yako ya siku ya leo, ni vizuri ukajiuliza maswali haya:
• Je
ni muda gani unaamka asubuhi?
• Je
unaweza kufanya nini kwanza kwa muda mfupi baada ya kuamka?
• Je
huwa unatumia dakika chache kutafakari ni mambo gani muhimu unataka kufanikisha
kwa siku?
• Je
huwa unatumia dakika 10 – 30 kila siku asubuhi kufanya mazoezi ya viungo ili
kunyoosha na kuweka mwili wako sawa?
Baada ya kujiuliza maswali yatakayokujenga kiakili
na kukusaidia kila siku kusogea karibu na mafanikio ya ndoto zako za maisha ni
muhimu kutilia mkazo yale uliyoazimia kuyafanya kwa siku ya leo haijalishi kuwa
ni madogo au makubwa, ni vyema ukawa mtendaji na sio mtu wa kuwaza sana bila
kutenda. Usidharau udogo wa kazi, ulichoorodhesha kufanya kwa siku ya leo
kinamaana kwako kwakuwa ulitafakari na kuandika chini mwenyewe nini unataka
kufanya kwa siku ya leo.
Siku ya leo inatakiwa kuwa ni yenye tija na
mafanikio makubwa kwako, fanya kazi zako zote za siku ya leo kwa furaha na kwa
uhodari. Siku iliokwenda vizuri kwako itahesabika kwa kuzaa matunda kutokana na
jitihada zako ulizoziweka katika kufanikisha yako malengo. Ifanye akili yako
iamini kile unachotaka kufanya kwa siku ya leo ni sahihi na kinawezekana, Kwa
kufanya hivyo utaongeza nguvu ya kufanya mambo yako kwa ufanisi na kwa nia
thabiti.
0 comments: